Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Wednesday, August 14, 2013

Kuongezeka kwa Maasi

Mathayo 24:12

Kwa kizazi cha zama hizi maasi yamekuwa ni jambo la kawaida sana, zaidi yamekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kila tunapokwenda na tunapokuwa maasi yanatuzunguka kiasi cha kuwanasa hata wanaoenenda katika njia ya haki.

Kuongezeka kwa maasi kunakwenda sambamba na upendo kupoa, na upendo unapopoa ndani yetu ina maana nafasi ya Mungu kwetu inakuwa haipo kwasababu Mungu ni pendo (1 Yohana 4:8), na kwa jinsi hii Shetani atatawala, kwakuwa nuru tena haipo.

Maasi huenea pale mwanadamu anapomsahau Mungu, akaanza ibada ya sanamu kwa kuvipa vitu vingine umuhimu na kipaumbele kuliko Mungu, ndipo anakuwa katika nafasi ya kufanya chochote kile ili kutimiza azma yake pasipokuwa na hofu yoyote juu ya Mungu wake aliyemuumba, yaani anakuwa amekufa kabisa kiroho ingawa katika mwili bado anaishi, na ikiendelea hivyo inafikia hatua ya kuamini kuwa hakuna Mungu kwasababu anaona yote anayafanikisha kwa uwezo na jitihada zake.

Inatisha sana pale maasi yanapotuteka watenda haki wa Mungu, na si kwamba yanatuteka kwakuwa yamekuwa na nguvu sana, hasha! (1 Yohana 4:4) Kwahiyo tunapofikia hatua ya kutekwa na uovu ina maana tumeamua kuchukuliana nao hata tukafikia hatua ya kutamani tukiona kuwa yamekuwa njia sahihi ya kuiendea.

Chanzo kikubwa sana cha maasi ni kupolomoka kwa maadili katika jamii, kiasi kwamba mambo ambayo yalikuwa ni aibu kuonekana yakifanyika sasa yanakubalika na kuwa jambo au tukio la kawaida kabisa. Badala ya kuzishika amri za Mungu, watu wanajisifia kwa kuzikiuka, na inaonekana kuwa ni jambo la kawaida kabisa. Mbaya zaidi wazazi wamekuwa mfano mbaya sana kwa watoto wao, ndio maana watoto wanajifunza kile wanachokiona kwa wazazi wao, na si vinginevyo.

Tunaweza kuepukana na maasi endapo tutaamua kubadilika tukimtafuta Mungu kwa bidii zote ili atuonyeshe namna ya kuenenda (Zaburi 32:8). Lakini pia inatupasa kujiweka mbali na kupenda pesa, maana ndiyo mwanzo wa maovu yote (1 Timotheo 6:10 | Mathayo 6:24).
Tunapofikia kujiona tuko kwenye hali salama, tukabweteka kwa sababu tumethibitisha tuko salama, lakini tutakuwa tumejiweka kwenye mtego mbaya sana kwa sababu bado hatujawa salama kama watoto wetu hawajaelimika wakakua katika misingi ya Mungu (Mithali 22:6). Zaidi ya hapo inabidi kuiombea na kuielimisha jamii yote kwa ujumla, maana sisi tumewekwa kuwa nuru ya ulimwengu.

Saturday, July 6, 2013

Kukubaliana na Mabadiliko

Mabadiliko kwa binadamu pamoja na mazingira yanayomzunguka ni kitu ambacho hakizuiliki kwani kilikuwepo, kipo na kitaendelea kuwepo kwa kadri ambavyo tunaishi katika dunia hii.
Kwa miaka mingi sana sasa, mambo mengi yamekuwa yakibadilika kwa maboresho tofauti tofauti, na kutokana na hili tunaona kuwa kuna mabadiliko yanayoleta maendeleo lakini pia kuna mabadiliko ambayo yanaturudisha nyuma ama kuharibu.

Mara nyingi mabadiliko yanapoanza kufanyika wengi tunajengwa katika hofu kwasababu asili ya miili yetu ni kuishi katika namna ambayo imezoea pia haipati shida, lakini kama ilivyo ada mabadiliko mengi huwa yanakuja katika namna ambayo si rahisi kukubalika moja kwa moja (Mwanzo 19:15 – 22).

Mungu anasababisha mabadiliko katika maisha yetu ili kutujenga, tuweze kuuona ukuu na uweza wake, pia kuweza kuliendea kusudi lake, na zaidi sana tusipoteze wakati katika maisha yetu.

Kukubaliana na mabadiliko ili kupelekea kusudi la Mungu katika maisha yetu kutimia ni utii na upendo (Isaya 1:19), lakini pia tumaini tukijua kuwa Mungu wetu ana mema kwa ajili yetu mbele ya safari, wala hanuwii mabaya kwa ajili yetu hata siku moja (Yeremia 29:11).

Katika majira tuliyo nayo, ni muhimu sana kubadilika kama ilivyo muhimu kukubaliana na kubadilika kwasababu ukombozi wetu uko karibu sana kipindi hiki kuliko pale mwanzo tulipoamini.

Hatuwezi kuendelea tukichukuliana tu na jamii inayotuzunguka kwa maovu na mambo yasiyofaa, kama ambavyo Lutu alichukuliana na jamii yake, lakini pia hakutaka kukimbilia milimani Mungu alipotaka aende kabla hajateketeza Sodoma na Gomora, bali katika mji wa Zoar (Mwanzo 19:18 – 20). Falsafa moja inasema kuwa dunia iko katika hali mbaya iliyonayo si kwa sababu ya wale wanaotenda maovu, bali wale wanaoyaona hayo maovu na kukaa kimya.

Yapo mambo na tabia tofauti tofauti ambazo watu wasiomjua Yesu wanaenenda kwayo, yamkini hata sisi kabla ya kumjua Yesu tulichotwa katika mkumbo huo (Wagalatia 5:19 – 21), lakini inasikitisha sana pale tunapogoma kubadilika na kuviacha tukisahau kabisa hayo mambo au tabia za mwili.

Tunapogoma kubadilika tunajiweka kwenye mazingira ya kuishi katika mwili, tena kujitengenezea milki zetu wenyewe hapa duniani ambako hakuna atakayeishi milele. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wengi wanataka kuendelea kubaki vijana siku zote, ndio maana kuna uvumbuzi mwingi sana kwa ajili ya kurekebisha ngozi, sura hata maumbo ili kurejea ujana.

Siri moja ya msingi ambayo wengi tunakosa kuifahamu ni kwamba Mungu peke yake ndiye habadiliki, lakini sisi wanadamu tuko safarini, hakika tunabadilika muda na siku zote. Mtu anayekua hawezi akaendelea kula chakula cha mtoto mdogo bali chakula kigumu kwa ajili ya mtu mzima (Waebrania 5:14).

Yule anayekubali kubadilika, Mungu anamuinua na kumtumia sana. Lakini ni vema kubadilika mapema kuliko kusubiri mabadiliko yakalazimishwa juu yetu au muda kusonga hata tusipate nafasi tena. Yule ambaye amechukua hatua ya kubadilika mapema, kwake inapokuja sheria ya kubadilika tayari yeye yuko juu ya sheria.


Thursday, July 4, 2013

Bwana Mungu Nashangaa Kabisa

1. Bwana Mungu, nashangaa kabisa
    Nikitazama kama vilivyo
    Nyota, ngurumo, vitu vingi vyote
    Viumbwavyo kwa uwezo wako.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

2. Nikitembea pote duniani,
    Ndege huimba, nawasikia,
    Milima hupendeza macho sana,
    Upepo nao nafurahia.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

3. Nikikumbuka kama wewe Mungu
    Ulivyompeleka Mwanao,
    Afe azichukue dhambi zetu,
    Kuyatambua ni vigumu mno.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

4. Yesu Mwokozi utakaporudi
    Kunichukua kwenda Mbinguni,
    Nitashukuru na kwimba milele
    Wote wajue jinsi ulivyo.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

Friday, June 28, 2013

Kuitambua Njia

Ni rahisi sana kujua njia inakutoa wapi na kukupeleka wapi, lakini inahitajika kazi ya ziada na umakini wa kutosha kutambua misukosuko iliyopo njiani. Dereva yeyote mzuri, anapopita njia kwa mara ya kwanza anakuwa makini sana, tofauti na anavyopita mara ya pili au zaidi maana tayari anajua hatari au vikwazo viko wapi, yaani amekuwa mzoefu.

Wana wa Israeli walitumia miaka 40 jangwani wakisafiri toka Misri kwenda Caanan katika njia ambayo iliwapasa kutumia siku 40 tu. Nataka kuamini kuwa umbali wa safari yao waliujua ila tu kwakuwa hawakujipanga kukabiliana na misukosuko pamoja na hatari zote wakimtumaini Mungu, ndio maana iliwangarimu miaka 40 badala ya siku 40 kwakuwa walikuwa wakilaumu na kulalamika katika kila ambacho walikosa.
Kutoka 16:2 – 3 | Hesabu 11:1 | Hesabu 14:1 – 4

Tofauti sana na Yusufu ambaye sio tu kufahamu, lakini pia alitambua njia aliyokuwa akiiendea, ndio maana tunamuona Yusufu akikataa kujihusisha kwenye uzinzi na mke wa Potifa. Yusufu aliamini kuwa ndoto alizoota (Mwanzo 37:6 – 11) hakika itakuwa kweli, naamini pia alijua kuwa siku zote yampasa kukaa na kudumu katika mpango wa Mungu akitenda mema.

Tulipokuwa, tulipo na tunapoelekea katika maisha yetu inawezekana tulitakiwa tuwe tumeshafika lakini bado yamkini hata safari hatujaianza kwakuwa tunafanya yote katika namna na kawaida ya jamii nzima. Lakini kuna ulemavu pia, maana mjinga akimuelimisha mjinga hakuna atakaye elimika. Kifaranga wa tai anapototolewa na kuku siku zote yeye atajiona kama kuku, wala si tai ingawa atakuwa tofauti kabisa na vifaranga wengine.

Ndio maana hazina kubwa hapa ulimwenguni haiko kwenye migodi, wala si kwenye benki ya dunia wala mashamba makubwa ya wakulima ila hazina kubwa ya dunia hii iko kwenye makaburi, ambapo ndimo walipozikwa watu ambao kama wangetambua njia wanayoiendea, basi dunia yetu leo ingekuwa ni mahali pa tofauti sana. 
Makaburini kuna falsafa nyingi, ugunduzi mpya wa maboresho, taaluma nyingi ambazo Mungu aliwapa hazina hao watu lakini kwa sababu moja au nyingine wametoweka mapema kwa kupita njia isiyofaa au waliamua kuishi maisha ya watu wengine. Hakika, mzabibu usiozaa matunda mazuri haufai tena ila kukatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 7:19

Inabidi kujiuliza leo kwamba tulipoanza safari hii, tulijua tunaelekea wapi, tuliitambua njia pamoja na kujiona kuwa tayari tumefika au lah! Haiba ya Mungu ni kuuona mwisho kutokea mwanzo (Isaya 46:10) hivyo kama tunaithibitisha tabia ya Mungu ndani yetu yatupasa kuuona mwisho tukiwa mwanzo.

Waebrania 11:1
Imani iliyo kamili ni kuwa na uhakika, yaani kushikilia kitu sio kwamba tukijua kuwa kitakuwa ila kuthibitisha kuwa kimeshakuwepo, kukiongea, kukitamka na kukiishi.
Zaidi sana katika yote tunayoenenda tukipanga na kufanya haitakiwi tuwe na haraka, maana Yakobo alikuwa na haraka kuwa na mke hatimaye akapewa dada wa mhusika (Mwanzo 29:15 – 30), lakini zaidi tukijali kuukomboa wakati.
Waefeso 5:15 – 16

Kitu kimoja, ambacho pia ni hazina ya msingi sana ni muda, na kwakutokutumia muda vema wengi tunapoteza sana muda tukifanya mambo yasiyo ya msingi.

Tuesday, June 25, 2013

Twonane Milele

1. Nyimbo na tuziimbe tena
    Za alivyotupenda mbele;
    Kwa damu ya thamani sana!
    Mbinguni hwonana milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
2. Hupozwa kila aoshwaye
    Kwa damu ya kondoo yule;
    Ataishi afurahiye
    Vya Yesu Mbinguni milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
3. Hata sasa hufurahia
    Tamu yake mapenzi yale,
    Je, kwake tukifikilia,
    Kutofarakana milele?
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
4. Twende mbele kwa jina lake
    Hata aje Mwokozi yule,
    Atatukaribisha kwake,
    Tutawale naye milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
5. Sauti zetu tuinue
    Kumsifu Mwokozi yule,
    Ili watu wote wajue
    Wokovu u kwake milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.

Monday, June 24, 2013

Kujishusha


Matatizo mengi katika jamii yetu yanatokana na kila mmoja kujiinua, kutaka kutambulika (umaarufu), pia kwasababu hatuna roho ya kujishusha.
Migogoro mingi katika familia ni kwa kuwa kina mama wanataka kuwa nafasi sawa na kina baba, wakijua kwamba wana uwezo wa kumudu majukumu, zaidi mpango wa haki sawa kwa wote umebadilisha kabisa maadili katika jamii nzima.
Mwanzo 3:16
Matatizo mengi katika maeneo ya kazi pia yanatokana na kutojishusha kwa mfanyakazi au mwajiriwa ambaye anaona anajua zaidi kuliko mkubwa wake, ama ni haki yake. Nakumbuka wakati mmoja mama yangu aliniambia kuwa “mwanangu mkubwa hakosei”, na si kwamba mama alimaanisha kuwa hakika mkubwa hakosei ila yampasa mdogo kushuka.
Mwanzo 39:11 – 19
Yusufu alikuwa na kila sababu ya kujitetea na kupignia haki yake, lakini aliamua kujishusha akiamini kwamba ndivyo inavyompasa kuenenda na kufanya, na hakika alimuona Mungu akimpigania na kumuinua hata alipokuwa gerezani.
Bwana wetu Yesu alijishusha sana hata kufikia mauti ya msalaba. Ingawa Yeye ni mfalme wa wafalme, lakini hakuishi katika jumba la kifaari, zaidi alipiga kambi na wanafunzi wake popote. Lakini pia, hata alipokamatwa, akateswa sana na kutemewa mate na kuishia msalabani, alisema “Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo”. Lakini, katika kujishusha kote huku ndipo tumepata wokovu mkuu na ulio wa thamani sana leo hii.
Mathayo 8:20 | Luka 23:34
Yakobo 4:10
Mtu anayejishusha siku zote Mungu humuinua sana. Zaidi, kujishusha ni kutohesabu vingapi tunapoteza ila kuachia kusudi la Mungu liweze kutimia katika maisha yetu. Mwizi anapokuja kuiba hazina yako ambayo Mungu alikusudia iwe yako, ataambulia kuchuma laana, lakini wewe utamuona Mungu akikubariki kwa hazina zaidi.
Warumi 12:20
Unapomsaidia adui kwa moyo mkunjufu, unakuwa umejishusha kwa kiasi kikubwa sana kwakuwa katika uhitaji wake kwa hali ya kawaida ndio wakati mzuri wa kulipa kisasi. Tukikumbuka Daudi alivyojishusha kwa Sauli mara mbili hata asimuue, na Mungu alimbariki na kumuinua Daudi.
Kujishusha kunaghairi mabaya, hata kosa likasamehewa na kusahaulika. Abigaili alivyojishusha na kumuokoa mumewe Nabali asiuliwe na Daudi, hata Daudi akakubali ombi na kughairi uteketezaji aliokuwa amenuia nyumbani kwa Nabal.
1 Samweli 25:23 – 35
Kujishusha ni tabia ya Mungu ndani yetu, hivyo tunapojishusha tunasababisha watu waione nuru ya Mungu ikiwaangazia, ndio maana mtume Paulo alijishusha sana katika huduma yake. Kujishusha hakutizami tunapoteza mangapi katika mwili bali tunaweka hazina kiasi gani Mbinguni kwa Baba yetu.

Hesabu Baraka


Maisha yetu kwa sehemu kubwa sana yamejawa na mtazamo wa kutizama ni kipi ambacho hatuna, ama ni wapi ambapo tunahangaika daima. Hakika duniani tunayo dhiki, lakini katika uhalisia tumebarikiwa sana kuliko dhiki tulizonazo, zaidi sana dhiki yetu ni ya kitambo kifupi tu.
Tunapohesabu baraka, tunaruhusu ukuu na uweza wa Mungu uonekane katika maisha yetu siku zote, zaidi tunaweza kuona na kujua kuwa Mungu yuko kazini akijishughulisha kwa ajili ya mambo yetu kuliko ambavyo tunaweza kutafakari na kuona.
Zaburi 100:4
Ukimtizama mtoto mdogo, anajua kuwa kila kitu kipo, tena anajua kuwa baba ana pesa ya kutosha kumnunulia kila anachohitaji, ndio maana siku zote watoto wana furaha na amani. Lakini pia watoto hawajui kupima uzito wa mahitaji muhimu, hivyo hatutakiwi kuwa kama watoto katika hili bali tutafakari siku zote mema ambayo Mungu ametufanyia na kushukuru tukimsifu daima.
Kubarikiwa si kuwa na majumba ya kifahari, wala magari na pesa nyingi bali kuwa mzima mwenye afya tele pamoja na amani ipitilizayo amani zote tukipata kibali kila tuendapo. Kubarikiwa pia ni kumjua sana Mungu tukizishika amri zake.
Ayubu 22:21
Mtu anapobarikiwa na Mungu, anatosheka anakuwa hana uhitaji tena, ndio maana Bwana Yesu alimwambia yule mwanamke Msamaria kuwa akinywa maji atakayompa Yeye hakika hataona kiu tena. Kitu chochote kile kilichobarikiwa na Mungu kinatosha kabisa wala hakihitaji nyongeza. Lakini tunapokuwa na mali ama utajiri ila tunahitaji kupata zaidi inabidi tujikague na kumuuliza Mungu kuwa ni baraka toka kwake au lah, kwa maana wengi wameacha kumuabudu Mungu wakaabudu mali na utajiri.
Yakobo 3:10
Mungu ametupa uwezo wa kujitamkia na kuwatamkia wengine laana au baraka, lakini mara nyingi tunatumia ndimi wetu kulaani badala ya kubariki. Mara nyingi tunajiambia kwamba hii kazi ikiisha sijui itakuwaje, ama siwezi kufanya biashara, au mke wangu ni mkorofi sana, ama watoto wangu ni wakaidi mno, au sidhani kama nitafanikiwa daima pamoja na mengine mengi. Haya pia huwa tunayazungumza kwa wengine hata tukawalaani.
Warumi 12:2
Kwa Mungu wetu hakuna laana, wala magomvi yoyote bali kuna amani, upendo, upole pamoja na baraka tele. Mataifa huenenda wakitizama nini au kipi wanakosa na wapi wamepungukiwa wakizidi kuona kwamba hakika maisha hayawatendei haki, bali sisi si wa dunia tena na haitupasi kuenenda kama wao.
Wafilipi 4:8
Inatupasa kutambua baraka zetu kama jinsi ambavyo zinatuzunguka, lakini pia inatubidi kukiri baraka hata kabla hatujaziona kwa macho ya nyama, cha msingi tumeshamuomba MUngu na kuamini hakika itakuwa sawa sawa na kuamini kwetu.