Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Sunday, September 18, 2011

Niite Nami Nitakuitikia

Neno la Mungu liko wazi sana, anasema niite nami nitakuitikia nakukuongesha mambo makubwa magumu usiyoyajua.
Katika maisha yetu ya kila siku tunapitia nyakati mbali mbali zinazotuweka katika kuwaza na kutafakari sana kwakuwa ni hali ambazo ziko nje sana ya uwezo wetu wa kuamua na kutenda, na kwa jinsi hii kuna ndugu zetu ambao wamefikia wasaa wa kutamka kuwa hakuna Mungu wakiamini kama yupo basi kwanini wateseke namna hiyo?
Nimejifunza kitu cha msingi sana kwamba Mungu anatupenda wote, na hataki yeyote aumie wala kupotea ila anataka sote tumuendee yeye tukitenda mapenzi yake daima, pia maandiko yanatuambia kuwa Mungu wetu humrudi yule ampendaye. Mungu anaweza kuruhusu magumu yatufike ili tuweze kujongea karibu naye zaidi kwakuwa hakuna gumu lolote linalomshinda yeye, maana vyote tunavyoviona vilifanyika kwa neno lake.
Si mara zote kwamba tunapofikwa na mabaya tumemkosema Mungu, hasha! bali inawezekana kabisa ni mpango wa Mungu pia kuikuza imani yetu ili kuona uthabiti uliomo ndani yetu maana Ayubu alikutwa na jaribu ambalo alishinda na Mungu akamuinua zaidi. Tunamkumbuka baba wa imani, Ibrahim ambaye aliambiwa na Mungu amtoe Isaka kuwa sadaka ya kuteketeza, na Mungu alitaka kupima kiwango cha imani ya Ibrahim. Maandiko yanasema pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu daima.
Imani huja kwa kusikia neno la Mungu hivyo ikakuwa na kutenda mambo makuu. Neno la Mungu ni chakula cha roho, usipisoma na kusikia neno la Mungu, wewe ni sawa na mtu mfu maana roho yako haina uhai bali imekufa, hivyo kwa namna hiyo unaenenda daima katika mwili wala si katika roho. Mungu ni roho, ndio maana Yesu akasema wakati unakuja na sasa upo ambao wamwabuduo halisi watamwabudu katika roho na kweli. Pia akasema tukiwa na imani kama chembe ya haradali, tunaweza kuuambia mlima ng'oka ukatupwe baharini nao ukatii.
Mungu ni mwema sana, anatupenda kuliko vyote maana yeye ni baba yetu hata kumtoa mwanaye wa pekee ili aje ajishushe kuliko malaika, afe kwa ajili yetu kupata ukombozi wa dhambi. Inabidi tuache sasa kuenenda kwa mazoea na kumfuata Yesu na kulitii neno lake siku zote ili Mungu akapate kwenda kuonekana katika maisha yetu na zaidi ya yote atupe kuurithi ufalme wa mbinguni.
Kumbuka dhahabu husafishwa kwenye moto hata ikatoka inang'aa sana, vivyo hivyo majaribu ni mtaji wa kukua kwa imani zetu. Mungu akubariki sana!