Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Saturday, September 8, 2012

Sheria Ya Mungu Ni Nzuri


Sheria zote alizoziweka Mungu wetu wa Mbinguni, ni mahususi ili kutulinda, zaidi sana ili tukaishi kwa furaha na amani pia tufanikiwe.
Mwanzo 2:16 – 17

Katika kila jambo, na kabla hatujafanya lolote lile yatupasa tukae chini na kutafakari kwanza, maana Mungu anasema hatuwezi neno lolote bila Yeye kwani Yeye anaufahamu mwanzo wetu tokea mwisho.

Kumbukumbu la Torati 5:13 – 14
Mungu amesema tufanye kazi siku sita, ya saba tupumzike akijua kabisa kwamba mwili katika uasilia wake unahitaji kupumzika, ili uwe na afya njema na kuweza kukabiliana na majukumu yanayofuata baada ya hapo.
Kinyume sana siku hizi tunafanya kazi mfululizo bila kupumzika, tukitumia vinywaji hata dawa zakusababisha nishati ya ziada mwilini, ndio maana watu wengi wana magonjwa ya moyo, kisukari, kansa na mengine mengi.

Kutoka 23:10 – 11
Ardhi inatakiwa ilimwe kwa miaka sita tu, na katika mwaka wa saba tunatakiwa tuiache ipumzike ili irejeshe rutuba, lakini sisi tumetizama njia mbadala ya kuweka kemikali tunazoziita mbolea ili uzalishaji uendelee siku zote kwa wingi, hivyo tunaishi na matokeo ya kula vyakula visivyo na virutubisho halisi kwa ajili ya miili yetu hata kupelekea maisha yetu kuwa mafupi zaidi kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kemikali hizi.

Neno la Mungu linapotuambia usizini wala kumtamani mwanamke asiye mke wako, ni ili kutuepusha na watoto wasiotarajiwa ambao wanaishia kuwa watoto wa mitaani ambao hawakupata pia hawapati malezi sahihi ya baba na mama, zaidi ukishazini unapoteza uthamani wako katika ubinadamu na taswira Mungu aliyotuumbia ndani yetu.
1 Wakorintho 6:18 – 20

Hakuna ambaye anataka kati yetu mke wake au mume wake atamaniwe na mtu mwingine, ambapo hili limekuwa tatizo sana katika maisha ya sasa hata watu kufikia hatua ya kuuana.

Unapoiba, unakuwa ni zaidi ya myonyaji kwani unachukua mali ambayo imetokana na jasho la mwenzako bure kabisa, na kwa namna hii tumeshuhudia wezi pamoja na majambazi wakichomwa moto na kuuliwa, maana hakuna anayekubali jasho lake liende bure awe mtumwa siku zote akiwanufaisha wengine.
Waefeso 4:28

Kwanini tumpende Mungu zaidi ya vyote na wote? Mungu ndiye muumba wetu, ndiye aliyetukomboa pia toka mikononi mwa shetani, lakini zaidi anatupatia na kututimizia mahitaji yetu ya kila siku hivyo Yeye tu ndiye anayepaswa kupewa upendo wote na heshima.
Mark 12:29 – 30

Tusipowaheshimu wazazi wetu ambao tunawaona, haiwezekani kumheshimu na kumpenda Mungu ambaye hatumuoni.

Wednesday, September 5, 2012

Maji Ya Uzima


Katika maisha ya mwanadamu awaye yoyote, lazima anakuwa na mahitaji tofauti tofauti kutokana na umri, tamaduni, mila pamoja na mazingira yanayomkabiri, lakini sote tunajua kuwa mwanadamu asilia ana mahitaji matatu muhimu ambayo ni chakula, nguo na malazi.

1 Timotheo 6:8
Ukitafakari kwa kina sana, wengi hatuangaiki ili kupata haya mahitaji matatu ya muhimu sana kwa kila mmoja wetu maana Mungu ndiye anayehakikisha kuwa katika hivi hatukosi chochote wala kupungukiwa. Ila siku zote tunahangaika sana kwa vitu vya kupita ambavyo siku zote kadri tunavyopata huwa hatutosheki hata siku moja.

Usasa na uvumbuzi wa mambo mengi tofauti unatuharibu sana wanadamu kwa sehemu kubwa badala ya kutusaidia, maana kila siku kuna aina mpya au kitu kipya ambacho siku zote unapotekwa hakika wewe unakuwa ukihaha bila kutosheka na kile ulichonacho, siku zote utahitaji zaidi.

Kuna mitindo ya nguo au viatu; inapotoka tu kila mtu anataka awe nayo ili aonekane anakwenda na wakati, hata kama atajaza kabati huyu mtu bado hatakuwa katosheka na vile alivyonavyo. Tizama hata simu, magari na vitu vingine hasa vinavyoonekana mbele za watu huwa havitupi kutosheka na kukubali kwa kile tulichonacho, lakini zaidi pia vijana wamekuwa wakibadilisha wenza wao kana kwamba ni bidhaa ya kununua dukani na kubadilisha kirahisi namna hivyo, yote ni kwa sababu hatutosheki na kile au yule tuliyenaye.
Mhubiri 1:7 – 8

Unapokula chakula au kunywa maji, unashiba au ile kiu inaisha kwa wakati huo lakini baada ya muda njaa au kiu itarejea tena. Tofauti sana kwa upande mwingine ambapo macho huwa hayachoki kuona hata siku moja, pua nazo hazichoki kunusa wala masikio hayachoki daima kusikia.

Ndio maana mlevi atalewa lakini atataka kuendelea kunywa tu, na mwizi hawezi kufikia wakati akasema sasa nimeshaiba inatosha, hapana. Mzinzi au mwasherati siku zote anapatwa na uhitaji wa kuendelea na matendo yake machafu kwakuwa hawezi kujizuia zaidi sana msukumo unakuwa ndani yake siku zote. Mtu mwenye mali nyingi siku zote hazimtoshi zaidi anaishi kwa hofu ya kupoteza zote hivyo daima anataka awenazo nyingi zaidi. Kwa yote ya mwili hakuna anayetosheka hata siku moja.

Yohana 4:5 – 18
Tumepata Tumaini la milele, Tumaini la kweli ambalo ni ushindi na habari njema kwa wote wanaosumbuka wakielemewa na njaa pamoja na kiu zisizokwisha maana Bwana wetu Yesu Kristo ana maji ya uzima, ambayo anatupatia bure, ila anachotaka kutoka kwetu ni kumuomba Yeye maji haya ya uzima ili tusisikie kiu wala njaa tena.

Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa! Lakini kizazi hiki kina njaa na kiu ya mitandao ya jamii, simu za mkononi, maisha ya anasa, ulevi pamoja na uzinzi na uasherati. Tumuombe sana Baba yetu wa mbinguni leo aondoe kiu nyingine zote kwetu na jamii nzima, na kujenga ndani yetu njaa na kiu ya haki.

Tuesday, August 28, 2012

Leteni Hoja Zenye Nguvu



Unapomwendea mwajiri wako katika hitaji lako, huwezi ukaenda tu nakumwambia hitaji lako bali inakupasa uende ukiwa umejipanaga vema kukabiliana na maswali atakayokuuliza. Vivyo hivyo, hata mzazi anapopelekewa hitaji na mwanaye, atahitaji kufahamu umuhimu pia ulazima wa yeye kutimiza lile hitaji.
Ndivyo ilivyo hata kwa Baba yetu wa Mbinguni, ambaye siku zote anahitaji twende kwake tukiwa na hoja zenye Nguvu, ili tupate kupewa hitaji letu.
Isaya 41:21

Katika maisha yetu ya wokovu, inawezekana kabisa hatuendi katika utimilifu unaotakiwa ndio maana hata tunapokuwa na mahitaji ya msingi ya kuyapeleka kwa Mungu hatuwezi kupokea maana hatuna hoja za msingi hasa za kuzifungamanisha.
Hakuna mzazi ambaye anajua kabisa mtoto wake bado hajakua vya kutosha akaanza kumkabidhi majukumu mazito au kumpa nyenzo zilizo nje ya uwezo wake.

Hezekia alipougua, hoja yake ya msingi mbele za Mungu ilikuwa kumkumbusha Mungu jinsi ambavyo alikwenda mbele zake kwa ukamilifu wote, hata Mungu akakumbuka na kumponya tena akamuongezea miaka kumi na tano ya kuishi.
Isaya 38:1 – 6

Wengi wetu inawezekana tumeshakutana na fulsa mbalimbali wakati tunakua, ambazo pia huwa tunaziendeleza kwa watoto wetu. Mzazi anapomwambia mwanaye akifaulu mtihani atamnunulia zawadi au kitu anachokipenda sana, na ikawa mtoto akajitahidi na kufaulu mtihani basi mzazi anakuwa kwenye msukumo mkubwa wa kutimiza ahadi yake. Zaidi sana kwa Mungu wetu, tunapoenenda katika ukamilifu wote Naye atatimiza ahadi zake kwetu.

Isaya 43:26
Unakuwa na ujasiri sana unapokwenda mahali kudai haki yako, hasa unajua kwamba hakika hiyo ni haki yako, zaidi sana Mungu wetu anatupenda na kutujali kuliko hata wazazi wetu wa hapa duniani.
Bwana Yesu anasema kwamba tukimkiri Yeye mbele za mataifa, hakika naye atatukiri mbele za Baba yake aliye mbinguni.
Mathayo 10:32 – 33

Kuna siri moja ya kumkiri Yesu mbele za watu siku zote. Mungu anatutizama katika uhalisia kwamba sisi tumebeba taswira yake, hivyo tunapomkiri mbele za watu kwa matendo na maneno yetu tunampa msukumo wa Yeye kufanya kitu katika maisha yetu siku zote.

Hatasiku moja huwezi kurudisha bidhaa feki kwenye kampuni halali, maana inapofika pale wao hawaitambui kwasababu haiku kwenye nakala zao. Hivyo haiwezekani ukawa unamkiri Yesu kwa mdomo tu bila matendo ukategemea ujenge hoja za hapa na pale katika hitaji lako naye akupatie sawasawa na kuhitaji kwako.
Mathayo 7:22 – 23

Wednesday, August 22, 2012

Uraia wa Mbinguni



Ukiwa ni mkazi wa mji ambao wanaishi watu toka sehemu za tofauti mwa taifa, ni rahisi sana kumgundua mgeni anayetoka mkoa mwingine hasa kwa lafudhi yake pia lugha, na zaidi sana mavazi.
Lakini picha nzuri unaipata ukitembelea au kama unaishi nchi ya ugenini, maana kwanza unajiona mgeni eneo lile lakini pia inakuwa rahisi sana kumgundua mgeni mwingine au mwenyeji pia kwani katika mataifa yote ya dunia tunatofautiana sana katika mavazi, lugha pia lafundi hata kama lugha ni ile ile lakini zaidi sana hata rangi.

Mathayo 3:1 – 2
Mtu ambaye hajatubu, hayuko katika utayari wa kuupokea ufalme wa Mungu, maana hajatengeneza mazingira halisi ya kuishi katika ufalme wa Mungu. Lakini pia hata ambaye ametubu inawezekana kabisa bado hajaupokea ufalme wa Mungu ila ndio anaelekea.

Unapoomba uraia wa nchi nyingine kuna vitu vingi sana wanavyokufanyia usaili kwavyo; kama nchi unayotoka, historia yako, elimu yako, kazi yako na kipato, ukubwa wa familia yako pamoja na dhumuni lako katika nchi hiyo. Na ni pale unapomudu vigezo vyote ndipo utakapoweza kupata uraia wa nchi ile.

Mathayo 4:17
Bwana wetu, Yesu Kristo aliuleta ufalme wa Mungu hapa duniani, ili tuupokee na kuishi tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Yesu ndiye mwanadamu pekee aliyeishi bila kutenda dhambi ingawa alijaribiwa hata zaidi ya tunavyojaribiwa leo hii.

Unapoupokea ufalme wa Mungu, kwako kuiba sio chaguo, wala kusema uongo si hatua ya kuifikia, tamaa haiwi tena sehemu ya maisha yako, ulevi wala uasherati vinakuwa si tena mvuto kwako zaidi kila kinachoitwa dhambi unakichukia sana maana unafurahi na kufarijika daima unapoishi katika ufalme wa Mungu. Hakuna mtu anayechukia nyumbani kwao, walipo ndugu na jamaa zake.
Raia wa nchi masikini anapokwenda kwenye nchi tajiri akafanikiwa sana na kupata kibali cha kuishi huko atafanya kila awezalo kuzishika na kutozivunja sheria za hiyo nchi kwani amepata sehemu ya furaha, faraja na amani pia.
Mathayo 13:44

Inatupasa tuutafute ufalme wa Mungu leo, maana inawezekana tumeokoka lakini bado tunashindana sana na dhambi kila inapoitwa leo, hata inafika wakati tunakata tamaa. Tufahamu kwamba kuokoka ni hatua ya msingi sana tuliyoifikia ila ili kumpendeza Mungu inabidi tuwe watakatifu, na hatuwezi kuwa watakatifu bila kuupokea ufalme Wake.
1 Peter 1:15 – 16

Mathayo 6:33 – 34
Tabia moja ya ufalme ni kuwa na kiongozi (mfalme) ambaye anahakikisha kila mtu anapata anachohitaji maana yeye ndiye anayemiliki wote na vyote. Sisi tunahangaikia sana maisha maana bado tunaamini sisi ni mali yetu wenyewe. Kama ambavyo mimi na wewe tunahudumia familia zetu je, si zaidi sana Baba yetu wa mbinguni?

Thursday, July 26, 2012

Kwa Mema na Mabaya



Ni vema kuchukua muda, na kujiuliza nia hasa za moyoni mwetu kumfuata Yesu maana inawezekana tukaamini kuwa tunamfuata Yesu kumbe tunaifuata njia yetu wenyewe bila kujua.
Je, tunaushikilia wokovu kwakuwa tunajua kuna hukumu inakuja, au kwakuuogopa moto wa milele? Haya yasingekuwepo tungeendelea kuupigania wokuvu na kuushikilia kwa lolote hata kufa?

Wengi wetu ambao tumefikia na watakaofikia maamuzi ya kuoa, tunasukumwa zaidi na tamaa zetu za mwili lakini si kwamba tuna upendo halisi ambao Mungu anataka tuwe nao; maana kuna ndoa nyingi sana ambazo zina migogoro au kuvunjika kabisa kwakuwa tu ule mvuto wa kimwili kwa mmoja au wote umepotea kabisa.
Mfanyakazi siku zote anaonekana mzuri sana hata akapewa sifa nyingi na kupendwa pale tu ambapo hakosei, lakini siku akikosea haijalishi kuna mangapi mazuri ameshafanya ila kama ilivyo haiba yetu binadamu tunasahau yote mazuri na kutizama kosa moja.

Yohana 14:15 Yesu anasema tukimpenda Yeye tutazishika amri zake.
Kuzishika amri zake ni kutekeleza tukitenda yale yote aliyotuagiza, haijalishi kwamba tunaonekanaje katika jamii bali tuonekane wenye haki kwake. Pia, haijalishi kuna mangapi tumekosa ila yatupasa kuing’ang’ania iliyo kweli yake.

Daniel 3:17 – 18
Shedrack, Meshack and Abed-Nego walimwambia mfalme Nebukadnezzer kuwa Mungu wao wanayemwamini atawaokoa na moto wa tanuru, lakini hata isipokuwa hivyo hawawezi kuanguka na kuisujudu sanamu aliyoisimamisha mfalme, maana walikuwa na uhakika na Mungu wa kweli ambaye wanamwamini na kumtumaini.

Inawezekana wengi wetu tupo katika wokuvu kwakuwa Mungu anaonekana jinsi anavyotubariki, zaidi sana hatujapungukiwa kwa sasa, lakini ikitokea tumepungukiwa inawezekana kabisa tusiweze kustahilimi tukamuasi Mungu mara moja.
Yohana 6: 26
Kwenye harusi za siku hizi, watu hawaendi kanisani kushuhudia ndoa halisi, ila wanakwenda ukumbini kwenye sherehe ambapo hakika wanajua watakula na kunywa hata miili yao itosheke. Pia kwenye ugonjwa au shida ni wachache wanaoonekana kuliko kwenye sherehe na furaha.

Ayubu hakumkataa Mungu, wala kutenda kosa kwa namna yoyote ile pale alipopatwa na majanga ya kuibiwa mali, watoto wake kufa na yeye mwenyewe kupata majipu mabaya sana, lakini alisimama imara akimtumainia Mungu. Mungu anatupenda wakati wote, tunapokuwanacho hata tusipokuwanacho kwani Yeye ndiye anayetupatia vyote maana ni mali yake Yeye.

Nataka nikupe moyo ndugu yangu, zaidi sana unapukuwa katika wakati mzuri usistarehe na kujisahau ila mtafute Mungu kwa bidii sana, kwani maombi yako yatafanyika akiba katika siku zijazo upitapo katika majaribu, na hakika Mungu atakuvusha na kukuokoa akikusimamisha tena, cha msingi ni kutokata tamaa katika mabaya yote.
Zaburi 30:5b

Sunday, July 22, 2012

Upendo wa Wengi Kupoa



Miaka ya nyuma wazee wetu waliweza kulala kwenye nyumba za udongo na nyasi ambazo hazina ulinzi kama ilivyo hivi leo, lakini zaidi ya kuamini pia walikuwa salama. Kuna watu wachache waliomiliki magari, hawakuhofu kuibiwa maana usiku walipaki magari yao nje ambako kulikuwa na usalama wa kutosha.
Leo tunaishi kwenye nyumba za matofali zilizo na madirisha pia milango ya chuma zikiwa na uzio wa umeme pamoja na walinzi lakini bado hatuko salama kabisa, kwanini?

Mathayo 24:12 “na kwasababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa”
Mtu yeyote anayetenda dhambi, na kuizoea hatimaye inakuwa ni sehemu ya maisha yake hivyo hawezi kuishi bila kuitenda. Katika maisha ya jamii ya leo, kupokea rushwa imekuwa ni kitu cha kawaida, zaidi tunapoangalia maadili ya jamii nzima yanavyopotoka wote tukiwa mashahidi jinsi ambavyo vijana wanavyojihusisha katika mahusiano ya mapenzi mapema. Katika mengi ambayo tunayaona ya kawaida na kuchukuliana nayo, ndivyo jinsi upendo katika jamii unavyotoweka.

2 Timotheo 3:1 – 5
Kizazi cha leo tumekuwa na roho ya mimi kwanza, watu tunajipenda zaidi wenyewe na kujijali kuliko wengine, na hakika ni nani kati yetu asiyependa fedha? Siku zote fedha ndiyo chanzo au msingi wa maovu yote maana aliye na pesa ndiye anayeheshimiwa akiweza pia hata kununua haki ya mtu mwingine, na kwa namna hii kilemba cha kiburi kinakuwa juu ya kichwa chake.

Kutoka 20:12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Tofauti kabisa heshima na utii kwa wazazi wetu havipo kabisa siku hizi, maana kama kijana anamahusiano ya kimapenzi na mtu anayeweza kumzaa haiwezekani heshima kwa wazazi wake ikawepo? Zaidi kama tumejaribu kutafakari siku hizi vijana ndio wanaokufa mapema zaidi kuliko watu wazima na wazee.

Kutokana na kuongezeka kwa uhalifu imekuwa ngumu sana kutoa msaada kwa yoyote, hasa tunapojua kwamba unaweza kuwa mwema lakini malipo yakawa tofauti kabisa, zaidi kukuumizwa na kurudishwa nyuma. Inasikitisha tunapofahamu ni mahusiano mangapi mtu ameshakuwanayo kabla hajaoa, pale tu anapojua jinsi inavyomuathiri katika maisha yake ya baadaye na ndoa yake kiasi kwamba ndoa nyingi hazidumu.

Kazi na masumbufu ya maisha yamechukua sehemu kubwa sana ya maisha yetu, hatuna muda wala kuona umuhimu wa kupendana na kujali tunapokuwa hai au katika shida na ugonjwa, lakini kwenye msiba tunakusanyika na kuonyesha masikitiko na huzuni. Kutokana na mizigo ya dhambi ukali umejengeka ndani yetu, kwa jambo dogo tunawekeana chuki ya maisha na kulaani tukidhani kwamba pesa ndilo jawabu la mambo yote.

Kama Yuda alivyomsaliti Yesu, ni kutokana na vitu vya kupita tu zaidi anasa zinatupelekea kusalitiana na kujenga chuki baina yetu. Ukifuatilia kwa karibu, jamii ya sasa tunapenda sana anasa maana imekuwa ni sehemu ya maisha. Tumekuwa tukikimbiza sana maisha kuliko ilivyo kawaida ili kupata kila kitu haraka haraka. Yeyote anayepanda katika mwili atavuna uharibifu, lakini yule anayepanda katika roho atavuna uzima wa milele.