Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Saturday, September 8, 2012

Sheria Ya Mungu Ni Nzuri


Sheria zote alizoziweka Mungu wetu wa Mbinguni, ni mahususi ili kutulinda, zaidi sana ili tukaishi kwa furaha na amani pia tufanikiwe.
Mwanzo 2:16 – 17

Katika kila jambo, na kabla hatujafanya lolote lile yatupasa tukae chini na kutafakari kwanza, maana Mungu anasema hatuwezi neno lolote bila Yeye kwani Yeye anaufahamu mwanzo wetu tokea mwisho.

Kumbukumbu la Torati 5:13 – 14
Mungu amesema tufanye kazi siku sita, ya saba tupumzike akijua kabisa kwamba mwili katika uasilia wake unahitaji kupumzika, ili uwe na afya njema na kuweza kukabiliana na majukumu yanayofuata baada ya hapo.
Kinyume sana siku hizi tunafanya kazi mfululizo bila kupumzika, tukitumia vinywaji hata dawa zakusababisha nishati ya ziada mwilini, ndio maana watu wengi wana magonjwa ya moyo, kisukari, kansa na mengine mengi.

Kutoka 23:10 – 11
Ardhi inatakiwa ilimwe kwa miaka sita tu, na katika mwaka wa saba tunatakiwa tuiache ipumzike ili irejeshe rutuba, lakini sisi tumetizama njia mbadala ya kuweka kemikali tunazoziita mbolea ili uzalishaji uendelee siku zote kwa wingi, hivyo tunaishi na matokeo ya kula vyakula visivyo na virutubisho halisi kwa ajili ya miili yetu hata kupelekea maisha yetu kuwa mafupi zaidi kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kemikali hizi.

Neno la Mungu linapotuambia usizini wala kumtamani mwanamke asiye mke wako, ni ili kutuepusha na watoto wasiotarajiwa ambao wanaishia kuwa watoto wa mitaani ambao hawakupata pia hawapati malezi sahihi ya baba na mama, zaidi ukishazini unapoteza uthamani wako katika ubinadamu na taswira Mungu aliyotuumbia ndani yetu.
1 Wakorintho 6:18 – 20

Hakuna ambaye anataka kati yetu mke wake au mume wake atamaniwe na mtu mwingine, ambapo hili limekuwa tatizo sana katika maisha ya sasa hata watu kufikia hatua ya kuuana.

Unapoiba, unakuwa ni zaidi ya myonyaji kwani unachukua mali ambayo imetokana na jasho la mwenzako bure kabisa, na kwa namna hii tumeshuhudia wezi pamoja na majambazi wakichomwa moto na kuuliwa, maana hakuna anayekubali jasho lake liende bure awe mtumwa siku zote akiwanufaisha wengine.
Waefeso 4:28

Kwanini tumpende Mungu zaidi ya vyote na wote? Mungu ndiye muumba wetu, ndiye aliyetukomboa pia toka mikononi mwa shetani, lakini zaidi anatupatia na kututimizia mahitaji yetu ya kila siku hivyo Yeye tu ndiye anayepaswa kupewa upendo wote na heshima.
Mark 12:29 – 30

Tusipowaheshimu wazazi wetu ambao tunawaona, haiwezekani kumheshimu na kumpenda Mungu ambaye hatumuoni.

Wednesday, September 5, 2012

Maji Ya Uzima


Katika maisha ya mwanadamu awaye yoyote, lazima anakuwa na mahitaji tofauti tofauti kutokana na umri, tamaduni, mila pamoja na mazingira yanayomkabiri, lakini sote tunajua kuwa mwanadamu asilia ana mahitaji matatu muhimu ambayo ni chakula, nguo na malazi.

1 Timotheo 6:8
Ukitafakari kwa kina sana, wengi hatuangaiki ili kupata haya mahitaji matatu ya muhimu sana kwa kila mmoja wetu maana Mungu ndiye anayehakikisha kuwa katika hivi hatukosi chochote wala kupungukiwa. Ila siku zote tunahangaika sana kwa vitu vya kupita ambavyo siku zote kadri tunavyopata huwa hatutosheki hata siku moja.

Usasa na uvumbuzi wa mambo mengi tofauti unatuharibu sana wanadamu kwa sehemu kubwa badala ya kutusaidia, maana kila siku kuna aina mpya au kitu kipya ambacho siku zote unapotekwa hakika wewe unakuwa ukihaha bila kutosheka na kile ulichonacho, siku zote utahitaji zaidi.

Kuna mitindo ya nguo au viatu; inapotoka tu kila mtu anataka awe nayo ili aonekane anakwenda na wakati, hata kama atajaza kabati huyu mtu bado hatakuwa katosheka na vile alivyonavyo. Tizama hata simu, magari na vitu vingine hasa vinavyoonekana mbele za watu huwa havitupi kutosheka na kukubali kwa kile tulichonacho, lakini zaidi pia vijana wamekuwa wakibadilisha wenza wao kana kwamba ni bidhaa ya kununua dukani na kubadilisha kirahisi namna hivyo, yote ni kwa sababu hatutosheki na kile au yule tuliyenaye.
Mhubiri 1:7 – 8

Unapokula chakula au kunywa maji, unashiba au ile kiu inaisha kwa wakati huo lakini baada ya muda njaa au kiu itarejea tena. Tofauti sana kwa upande mwingine ambapo macho huwa hayachoki kuona hata siku moja, pua nazo hazichoki kunusa wala masikio hayachoki daima kusikia.

Ndio maana mlevi atalewa lakini atataka kuendelea kunywa tu, na mwizi hawezi kufikia wakati akasema sasa nimeshaiba inatosha, hapana. Mzinzi au mwasherati siku zote anapatwa na uhitaji wa kuendelea na matendo yake machafu kwakuwa hawezi kujizuia zaidi sana msukumo unakuwa ndani yake siku zote. Mtu mwenye mali nyingi siku zote hazimtoshi zaidi anaishi kwa hofu ya kupoteza zote hivyo daima anataka awenazo nyingi zaidi. Kwa yote ya mwili hakuna anayetosheka hata siku moja.

Yohana 4:5 – 18
Tumepata Tumaini la milele, Tumaini la kweli ambalo ni ushindi na habari njema kwa wote wanaosumbuka wakielemewa na njaa pamoja na kiu zisizokwisha maana Bwana wetu Yesu Kristo ana maji ya uzima, ambayo anatupatia bure, ila anachotaka kutoka kwetu ni kumuomba Yeye maji haya ya uzima ili tusisikie kiu wala njaa tena.

Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa! Lakini kizazi hiki kina njaa na kiu ya mitandao ya jamii, simu za mkononi, maisha ya anasa, ulevi pamoja na uzinzi na uasherati. Tumuombe sana Baba yetu wa mbinguni leo aondoe kiu nyingine zote kwetu na jamii nzima, na kujenga ndani yetu njaa na kiu ya haki.