Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Wednesday, May 2, 2012

Maamuzi


Maamuzi ni kitu cha msingi sana katika maisha ya mwanadamu hasa kama yanafanyika kwa Hekima, Busara pamoja na usahihi; kwanini? Kwasababu maamuzi unayoyafanya sasa itakubidi uishi matokeo yake baadaye. Ukiamua jambo Fulani, au usiamue vyovyote kwa namna hiyo bado unakuwa umefanya maamuzi hakika.

Waamuzi 16:17 – 21 Samsoni aliamua kufanya maamuzi ya kuvunja unadhiri wake kwa Mungu kwasababu alimpenda sana Delila, lakini hakika ilimgharimu Samsoni kusudi la Mungu ndani yake, macho yake hata uhuru wake.Unaposhindwa kufanya maamuzi sahihi siku zote unakuwa mtumwa.
Kati yetu kuna ambaye hajawahi kuwa kwenye hali ambayo ni ngumu sana, kutokana na maamuzi yasiyofaa uliyoyafanya hata akahisi kabisa kwamba ndani yako uwepo wa Mungu haupo kabisa kiasi kwamba hata maombi yake ni kama yanamzunguka tu hayaendi popote?
Kuna dada zetu ambao wanadanganywa na kina kaka ambao hata hawaeleweki kuwa na muelekeo mzuri wa maisha; ni pale anapoambiwa tu “NAKUPENDA” anaona vingine vyote havifai, kiasi cha kufikia hatua ya kuukimbia wokovu. Katika maamuzi kama haya siku zote huwa hatuhesabu gharama kabla ya kuchukua hatua. Luka 14:28 – 30
Mwana Mpotevu aliamua kuchukua urithi wake toka kwa baba yake, akaenda kuishi maisha ya anasa na kutumia mali zote hata zikaisha; akaishia kwenye kazi ya kulisha nguruwe hata kutamani kushiriki chakula na nguruwe. Luka 15:11 – 21
Ndio maana dhambi ni kitu kibaya sana, kwani unakuja kujua na kujutia maamuzi uliyofanya baadaye, pia inatubidi tufahamu kuwa si mara zote utajuta hapa duniani bali kuna wakati utajuta kwenye moto wa milele.
Maamuzi ya Eva kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya pia akamshawishi mumewe Adam ambaye naye aliamua kushiriki na mkewe viliwagharimu sana, ambapo kwa dhambi hiyo inatugharimu hata sisi leo hii. Lakini, Bwana Yesu aliamua kuja duniani ateseke, afe na afufuke ili sisi tupate msamaha wa dhambi kwa kupitia Yeye, hivyo badala ya sisi kuhukumiwa tupate kuhesabiwa haki yote.Yohana 3:16 – 17
Isaya 46:10 Mungu pekee ndiye anayefahamu siri ya mambo yajayo, dakika chache hata miaka kenda inayokuja mpaka milele yote. Siku zote tunapofanya maamuzi, kama hatuongozwi na Roho wa Mungu hakika tuna nafasi kubwa sana ya kukosea na kuishi katika majuto.
Kuna watu ambao wanafahamika kuwa na busara pia Hekima sana za kibinadamu, ila hawa pia wamekosea na wataendelea kukosema katika mambo tofauti tofauti kwani Mungu amewaficha wazee wenye Hekima akawafunulia watoto wadogo. Mathayo 11:25
Ukiamka asubuhi anza na Yesu, ukitaka kufanya jambo mshirikishe Yeye wala usitizame urahisi wa jambo au mara ngapi umeshalifanya kwani sisi hukosea daima na haijalishi, ila Yesu ni yule yule jana leo na hata milele, na hajawahi wala haitatokea akakosea kamwe. Malachi 3:6