Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Wednesday, August 14, 2013

Kuongezeka kwa Maasi

Mathayo 24:12

Kwa kizazi cha zama hizi maasi yamekuwa ni jambo la kawaida sana, zaidi yamekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kila tunapokwenda na tunapokuwa maasi yanatuzunguka kiasi cha kuwanasa hata wanaoenenda katika njia ya haki.

Kuongezeka kwa maasi kunakwenda sambamba na upendo kupoa, na upendo unapopoa ndani yetu ina maana nafasi ya Mungu kwetu inakuwa haipo kwasababu Mungu ni pendo (1 Yohana 4:8), na kwa jinsi hii Shetani atatawala, kwakuwa nuru tena haipo.

Maasi huenea pale mwanadamu anapomsahau Mungu, akaanza ibada ya sanamu kwa kuvipa vitu vingine umuhimu na kipaumbele kuliko Mungu, ndipo anakuwa katika nafasi ya kufanya chochote kile ili kutimiza azma yake pasipokuwa na hofu yoyote juu ya Mungu wake aliyemuumba, yaani anakuwa amekufa kabisa kiroho ingawa katika mwili bado anaishi, na ikiendelea hivyo inafikia hatua ya kuamini kuwa hakuna Mungu kwasababu anaona yote anayafanikisha kwa uwezo na jitihada zake.

Inatisha sana pale maasi yanapotuteka watenda haki wa Mungu, na si kwamba yanatuteka kwakuwa yamekuwa na nguvu sana, hasha! (1 Yohana 4:4) Kwahiyo tunapofikia hatua ya kutekwa na uovu ina maana tumeamua kuchukuliana nao hata tukafikia hatua ya kutamani tukiona kuwa yamekuwa njia sahihi ya kuiendea.

Chanzo kikubwa sana cha maasi ni kupolomoka kwa maadili katika jamii, kiasi kwamba mambo ambayo yalikuwa ni aibu kuonekana yakifanyika sasa yanakubalika na kuwa jambo au tukio la kawaida kabisa. Badala ya kuzishika amri za Mungu, watu wanajisifia kwa kuzikiuka, na inaonekana kuwa ni jambo la kawaida kabisa. Mbaya zaidi wazazi wamekuwa mfano mbaya sana kwa watoto wao, ndio maana watoto wanajifunza kile wanachokiona kwa wazazi wao, na si vinginevyo.

Tunaweza kuepukana na maasi endapo tutaamua kubadilika tukimtafuta Mungu kwa bidii zote ili atuonyeshe namna ya kuenenda (Zaburi 32:8). Lakini pia inatupasa kujiweka mbali na kupenda pesa, maana ndiyo mwanzo wa maovu yote (1 Timotheo 6:10 | Mathayo 6:24).
Tunapofikia kujiona tuko kwenye hali salama, tukabweteka kwa sababu tumethibitisha tuko salama, lakini tutakuwa tumejiweka kwenye mtego mbaya sana kwa sababu bado hatujawa salama kama watoto wetu hawajaelimika wakakua katika misingi ya Mungu (Mithali 22:6). Zaidi ya hapo inabidi kuiombea na kuielimisha jamii yote kwa ujumla, maana sisi tumewekwa kuwa nuru ya ulimwengu.