Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Saturday, July 6, 2013

Kukubaliana na Mabadiliko

Mabadiliko kwa binadamu pamoja na mazingira yanayomzunguka ni kitu ambacho hakizuiliki kwani kilikuwepo, kipo na kitaendelea kuwepo kwa kadri ambavyo tunaishi katika dunia hii.
Kwa miaka mingi sana sasa, mambo mengi yamekuwa yakibadilika kwa maboresho tofauti tofauti, na kutokana na hili tunaona kuwa kuna mabadiliko yanayoleta maendeleo lakini pia kuna mabadiliko ambayo yanaturudisha nyuma ama kuharibu.

Mara nyingi mabadiliko yanapoanza kufanyika wengi tunajengwa katika hofu kwasababu asili ya miili yetu ni kuishi katika namna ambayo imezoea pia haipati shida, lakini kama ilivyo ada mabadiliko mengi huwa yanakuja katika namna ambayo si rahisi kukubalika moja kwa moja (Mwanzo 19:15 – 22).

Mungu anasababisha mabadiliko katika maisha yetu ili kutujenga, tuweze kuuona ukuu na uweza wake, pia kuweza kuliendea kusudi lake, na zaidi sana tusipoteze wakati katika maisha yetu.

Kukubaliana na mabadiliko ili kupelekea kusudi la Mungu katika maisha yetu kutimia ni utii na upendo (Isaya 1:19), lakini pia tumaini tukijua kuwa Mungu wetu ana mema kwa ajili yetu mbele ya safari, wala hanuwii mabaya kwa ajili yetu hata siku moja (Yeremia 29:11).

Katika majira tuliyo nayo, ni muhimu sana kubadilika kama ilivyo muhimu kukubaliana na kubadilika kwasababu ukombozi wetu uko karibu sana kipindi hiki kuliko pale mwanzo tulipoamini.

Hatuwezi kuendelea tukichukuliana tu na jamii inayotuzunguka kwa maovu na mambo yasiyofaa, kama ambavyo Lutu alichukuliana na jamii yake, lakini pia hakutaka kukimbilia milimani Mungu alipotaka aende kabla hajateketeza Sodoma na Gomora, bali katika mji wa Zoar (Mwanzo 19:18 – 20). Falsafa moja inasema kuwa dunia iko katika hali mbaya iliyonayo si kwa sababu ya wale wanaotenda maovu, bali wale wanaoyaona hayo maovu na kukaa kimya.

Yapo mambo na tabia tofauti tofauti ambazo watu wasiomjua Yesu wanaenenda kwayo, yamkini hata sisi kabla ya kumjua Yesu tulichotwa katika mkumbo huo (Wagalatia 5:19 – 21), lakini inasikitisha sana pale tunapogoma kubadilika na kuviacha tukisahau kabisa hayo mambo au tabia za mwili.

Tunapogoma kubadilika tunajiweka kwenye mazingira ya kuishi katika mwili, tena kujitengenezea milki zetu wenyewe hapa duniani ambako hakuna atakayeishi milele. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wengi wanataka kuendelea kubaki vijana siku zote, ndio maana kuna uvumbuzi mwingi sana kwa ajili ya kurekebisha ngozi, sura hata maumbo ili kurejea ujana.

Siri moja ya msingi ambayo wengi tunakosa kuifahamu ni kwamba Mungu peke yake ndiye habadiliki, lakini sisi wanadamu tuko safarini, hakika tunabadilika muda na siku zote. Mtu anayekua hawezi akaendelea kula chakula cha mtoto mdogo bali chakula kigumu kwa ajili ya mtu mzima (Waebrania 5:14).

Yule anayekubali kubadilika, Mungu anamuinua na kumtumia sana. Lakini ni vema kubadilika mapema kuliko kusubiri mabadiliko yakalazimishwa juu yetu au muda kusonga hata tusipate nafasi tena. Yule ambaye amechukua hatua ya kubadilika mapema, kwake inapokuja sheria ya kubadilika tayari yeye yuko juu ya sheria.


Thursday, July 4, 2013

Bwana Mungu Nashangaa Kabisa

1. Bwana Mungu, nashangaa kabisa
    Nikitazama kama vilivyo
    Nyota, ngurumo, vitu vingi vyote
    Viumbwavyo kwa uwezo wako.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

2. Nikitembea pote duniani,
    Ndege huimba, nawasikia,
    Milima hupendeza macho sana,
    Upepo nao nafurahia.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

3. Nikikumbuka kama wewe Mungu
    Ulivyompeleka Mwanao,
    Afe azichukue dhambi zetu,
    Kuyatambua ni vigumu mno.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.

4. Yesu Mwokozi utakaporudi
    Kunichukua kwenda Mbinguni,
    Nitashukuru na kwimba milele
    Wote wajue jinsi ulivyo.

Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu,
Roho yangu na ikuimbie
Jinsi wewe ulivyo Mkuu.