Mabadiliko
kwa binadamu pamoja na mazingira yanayomzunguka ni kitu ambacho hakizuiliki
kwani kilikuwepo, kipo na kitaendelea kuwepo kwa kadri ambavyo tunaishi katika
dunia hii.
Kwa miaka mingi sana sasa, mambo mengi yamekuwa yakibadilika
kwa maboresho tofauti tofauti, na kutokana na hili tunaona kuwa kuna mabadiliko
yanayoleta maendeleo lakini pia kuna mabadiliko ambayo yanaturudisha nyuma ama
kuharibu.
Mara nyingi mabadiliko yanapoanza kufanyika wengi tunajengwa
katika hofu kwasababu asili ya miili yetu ni kuishi katika namna ambayo imezoea
pia haipati shida, lakini kama ilivyo ada mabadiliko mengi huwa yanakuja katika
namna ambayo si rahisi kukubalika moja kwa moja (Mwanzo 19:15 – 22).
Mungu anasababisha mabadiliko katika maisha yetu ili
kutujenga, tuweze kuuona ukuu na uweza wake, pia kuweza kuliendea kusudi lake,
na zaidi sana tusipoteze wakati katika maisha yetu.
Kukubaliana na mabadiliko ili kupelekea kusudi la Mungu
katika maisha yetu kutimia ni utii na upendo (Isaya 1:19), lakini pia tumaini tukijua kuwa Mungu wetu ana mema
kwa ajili yetu mbele ya safari, wala hanuwii mabaya kwa ajili yetu hata siku
moja (Yeremia 29:11).
Katika majira tuliyo nayo, ni muhimu sana kubadilika kama
ilivyo muhimu kukubaliana na kubadilika kwasababu ukombozi wetu uko karibu sana
kipindi hiki kuliko pale mwanzo tulipoamini.
Hatuwezi kuendelea tukichukuliana tu na jamii inayotuzunguka
kwa maovu na mambo yasiyofaa, kama ambavyo Lutu alichukuliana na jamii yake,
lakini pia hakutaka kukimbilia milimani Mungu alipotaka aende kabla hajateketeza
Sodoma na Gomora, bali katika mji wa Zoar (Mwanzo
19:18 – 20). Falsafa moja inasema kuwa dunia iko katika hali mbaya
iliyonayo si kwa sababu ya wale wanaotenda maovu, bali wale wanaoyaona hayo
maovu na kukaa kimya.
Yapo mambo na tabia tofauti tofauti ambazo watu wasiomjua
Yesu wanaenenda kwayo, yamkini hata sisi kabla ya kumjua Yesu tulichotwa katika
mkumbo huo (Wagalatia 5:19 – 21),
lakini inasikitisha sana pale tunapogoma kubadilika na kuviacha tukisahau kabisa
hayo mambo au tabia za mwili.
Tunapogoma kubadilika tunajiweka kwenye mazingira ya kuishi
katika mwili, tena kujitengenezea milki zetu wenyewe hapa duniani ambako hakuna
atakayeishi milele. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wengi wanataka kuendelea
kubaki vijana siku zote, ndio maana kuna uvumbuzi mwingi sana kwa ajili ya
kurekebisha ngozi, sura hata maumbo ili kurejea ujana.
Siri moja ya msingi ambayo wengi tunakosa kuifahamu ni kwamba Mungu peke yake ndiye habadiliki, lakini sisi wanadamu tuko safarini, hakika tunabadilika muda na siku zote. Mtu anayekua hawezi akaendelea kula chakula cha mtoto mdogo bali chakula kigumu kwa ajili ya mtu mzima (Waebrania 5:14).
Yule anayekubali kubadilika, Mungu anamuinua na kumtumia
sana. Lakini ni vema kubadilika mapema kuliko kusubiri mabadiliko
yakalazimishwa juu yetu au muda kusonga hata tusipate nafasi tena. Yule ambaye
amechukua hatua ya kubadilika mapema, kwake inapokuja sheria ya kubadilika
tayari yeye yuko juu ya sheria.
No comments:
Post a Comment