Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Thursday, July 26, 2012

Kwa Mema na Mabaya



Ni vema kuchukua muda, na kujiuliza nia hasa za moyoni mwetu kumfuata Yesu maana inawezekana tukaamini kuwa tunamfuata Yesu kumbe tunaifuata njia yetu wenyewe bila kujua.
Je, tunaushikilia wokovu kwakuwa tunajua kuna hukumu inakuja, au kwakuuogopa moto wa milele? Haya yasingekuwepo tungeendelea kuupigania wokuvu na kuushikilia kwa lolote hata kufa?

Wengi wetu ambao tumefikia na watakaofikia maamuzi ya kuoa, tunasukumwa zaidi na tamaa zetu za mwili lakini si kwamba tuna upendo halisi ambao Mungu anataka tuwe nao; maana kuna ndoa nyingi sana ambazo zina migogoro au kuvunjika kabisa kwakuwa tu ule mvuto wa kimwili kwa mmoja au wote umepotea kabisa.
Mfanyakazi siku zote anaonekana mzuri sana hata akapewa sifa nyingi na kupendwa pale tu ambapo hakosei, lakini siku akikosea haijalishi kuna mangapi mazuri ameshafanya ila kama ilivyo haiba yetu binadamu tunasahau yote mazuri na kutizama kosa moja.

Yohana 14:15 Yesu anasema tukimpenda Yeye tutazishika amri zake.
Kuzishika amri zake ni kutekeleza tukitenda yale yote aliyotuagiza, haijalishi kwamba tunaonekanaje katika jamii bali tuonekane wenye haki kwake. Pia, haijalishi kuna mangapi tumekosa ila yatupasa kuing’ang’ania iliyo kweli yake.

Daniel 3:17 – 18
Shedrack, Meshack and Abed-Nego walimwambia mfalme Nebukadnezzer kuwa Mungu wao wanayemwamini atawaokoa na moto wa tanuru, lakini hata isipokuwa hivyo hawawezi kuanguka na kuisujudu sanamu aliyoisimamisha mfalme, maana walikuwa na uhakika na Mungu wa kweli ambaye wanamwamini na kumtumaini.

Inawezekana wengi wetu tupo katika wokuvu kwakuwa Mungu anaonekana jinsi anavyotubariki, zaidi sana hatujapungukiwa kwa sasa, lakini ikitokea tumepungukiwa inawezekana kabisa tusiweze kustahilimi tukamuasi Mungu mara moja.
Yohana 6: 26
Kwenye harusi za siku hizi, watu hawaendi kanisani kushuhudia ndoa halisi, ila wanakwenda ukumbini kwenye sherehe ambapo hakika wanajua watakula na kunywa hata miili yao itosheke. Pia kwenye ugonjwa au shida ni wachache wanaoonekana kuliko kwenye sherehe na furaha.

Ayubu hakumkataa Mungu, wala kutenda kosa kwa namna yoyote ile pale alipopatwa na majanga ya kuibiwa mali, watoto wake kufa na yeye mwenyewe kupata majipu mabaya sana, lakini alisimama imara akimtumainia Mungu. Mungu anatupenda wakati wote, tunapokuwanacho hata tusipokuwanacho kwani Yeye ndiye anayetupatia vyote maana ni mali yake Yeye.

Nataka nikupe moyo ndugu yangu, zaidi sana unapukuwa katika wakati mzuri usistarehe na kujisahau ila mtafute Mungu kwa bidii sana, kwani maombi yako yatafanyika akiba katika siku zijazo upitapo katika majaribu, na hakika Mungu atakuvusha na kukuokoa akikusimamisha tena, cha msingi ni kutokata tamaa katika mabaya yote.
Zaburi 30:5b

Sunday, July 22, 2012

Upendo wa Wengi Kupoa



Miaka ya nyuma wazee wetu waliweza kulala kwenye nyumba za udongo na nyasi ambazo hazina ulinzi kama ilivyo hivi leo, lakini zaidi ya kuamini pia walikuwa salama. Kuna watu wachache waliomiliki magari, hawakuhofu kuibiwa maana usiku walipaki magari yao nje ambako kulikuwa na usalama wa kutosha.
Leo tunaishi kwenye nyumba za matofali zilizo na madirisha pia milango ya chuma zikiwa na uzio wa umeme pamoja na walinzi lakini bado hatuko salama kabisa, kwanini?

Mathayo 24:12 “na kwasababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa”
Mtu yeyote anayetenda dhambi, na kuizoea hatimaye inakuwa ni sehemu ya maisha yake hivyo hawezi kuishi bila kuitenda. Katika maisha ya jamii ya leo, kupokea rushwa imekuwa ni kitu cha kawaida, zaidi tunapoangalia maadili ya jamii nzima yanavyopotoka wote tukiwa mashahidi jinsi ambavyo vijana wanavyojihusisha katika mahusiano ya mapenzi mapema. Katika mengi ambayo tunayaona ya kawaida na kuchukuliana nayo, ndivyo jinsi upendo katika jamii unavyotoweka.

2 Timotheo 3:1 – 5
Kizazi cha leo tumekuwa na roho ya mimi kwanza, watu tunajipenda zaidi wenyewe na kujijali kuliko wengine, na hakika ni nani kati yetu asiyependa fedha? Siku zote fedha ndiyo chanzo au msingi wa maovu yote maana aliye na pesa ndiye anayeheshimiwa akiweza pia hata kununua haki ya mtu mwingine, na kwa namna hii kilemba cha kiburi kinakuwa juu ya kichwa chake.

Kutoka 20:12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Tofauti kabisa heshima na utii kwa wazazi wetu havipo kabisa siku hizi, maana kama kijana anamahusiano ya kimapenzi na mtu anayeweza kumzaa haiwezekani heshima kwa wazazi wake ikawepo? Zaidi kama tumejaribu kutafakari siku hizi vijana ndio wanaokufa mapema zaidi kuliko watu wazima na wazee.

Kutokana na kuongezeka kwa uhalifu imekuwa ngumu sana kutoa msaada kwa yoyote, hasa tunapojua kwamba unaweza kuwa mwema lakini malipo yakawa tofauti kabisa, zaidi kukuumizwa na kurudishwa nyuma. Inasikitisha tunapofahamu ni mahusiano mangapi mtu ameshakuwanayo kabla hajaoa, pale tu anapojua jinsi inavyomuathiri katika maisha yake ya baadaye na ndoa yake kiasi kwamba ndoa nyingi hazidumu.

Kazi na masumbufu ya maisha yamechukua sehemu kubwa sana ya maisha yetu, hatuna muda wala kuona umuhimu wa kupendana na kujali tunapokuwa hai au katika shida na ugonjwa, lakini kwenye msiba tunakusanyika na kuonyesha masikitiko na huzuni. Kutokana na mizigo ya dhambi ukali umejengeka ndani yetu, kwa jambo dogo tunawekeana chuki ya maisha na kulaani tukidhani kwamba pesa ndilo jawabu la mambo yote.

Kama Yuda alivyomsaliti Yesu, ni kutokana na vitu vya kupita tu zaidi anasa zinatupelekea kusalitiana na kujenga chuki baina yetu. Ukifuatilia kwa karibu, jamii ya sasa tunapenda sana anasa maana imekuwa ni sehemu ya maisha. Tumekuwa tukikimbiza sana maisha kuliko ilivyo kawaida ili kupata kila kitu haraka haraka. Yeyote anayepanda katika mwili atavuna uharibifu, lakini yule anayepanda katika roho atavuna uzima wa milele.

Sunday, July 1, 2012

Mungu Anayetenda Makuu



Wapendwa wengi haitupi shida kuamini bila mashaka kwamba Mungu anaweza kutenda yote, na wala hakuna gumu linalomshinda kwakuwa tunaona mengi makuu aliyofanya pia anayoendelea kufanya Mungu kwa wengine, lakini sisi tunaona kwamba jambo kama hilo kutimia kwetu ni ngumu zaidi.

Muujiza siku zote ni kwa mwanadamu, lakini kwa Mungu sio muujiza kwani kwake yeye ni jambo la kutamka tu na inakuwa. Yamkini kuna miujiza mingi sana ambayo Mungu anatutendea katika maisha yetu ila tu huwa hatujaribu kutafakari na kumuuliza Mungu tukajua yale yaliyo sirini.

Jeremia 33:3
Dada mmoja alichelewa kuamka kwenda kazini, ingawa anaweka kengele ya kumuamsha siku zote lakini hauisikia, hata ilipofika mchana chakula chake kilicheleweshwa sana, zaidi aliporudi nyumbani akajaribu kupumzika na kuweka miguu yake kwenye kifaa cha kukanda miguu ambacho hakikufanya kazi. Huyu dada alihuzunika sana akimuuliza Mungu kwanini kila kitu hakijaenda sawa siku hiyo. Mungu akamwambia alimsababisha achelewe kazini kwa sababu kulikuwa na dereva mlevi njiani ambaye angemsababishia ajali pengine kupoteza maisha, pia chakula kilichelewa kwakuwa aliyekiandaa mwanzo alikuwa anaumwa ugonjwa wa kuambukiza na mwisho, ile mashine ya kukanda miguu ilikuwa na tatizo ambalo lingesababisha nyumba yote ikose umeme.

Tukirejea kwa wana wa Israel ambao Mungu alikuwa nao akiwaongoza kutoka utumwani Misri ambako Alifanya mambo makubwa sana kwa namna tofauti hata Farao akawaachia huru, lakini zaidi sana aliwavusha bahari ya Sham, akawalisha mana na kwele jangwani, ila kutokana na kusahau kwao na ukaidi, Mungu anamwambia Musa kwamba watu hawa wana shingo ngumu.
Kutoka 32:9

Wote tunafahamu kuhusu ajali hasa za magari ambazo huwa zinatokea, kiasi kwamba ukiona gari lilivyo unasema hakika hapa hakuna mtu aliyetoka mzima ila kwa mshangao wetu tunaambia kwamba wote waliokuwemo wametoka wazima wakiwa na michubuko tu.
Mbali ya kwamba Mungu ana makusudi kwa kila jambo, hakika ukifikia viwango vya kupata baraka utazipata tu haijalishi unazitaka au huzitaki, vivyo hivyo ukifikia viwango vya kupata muujiza utaupata tu bila kujali unauhitaji au lah.
Isaya 43:26

Tumesahau kuna wangapi wamekufa wakiwa watoto wadogo kabisa, au hatujaona ukuu wa Mungu tuko hai hata leo sio wagonjwa wala kuwa na ulemavu wowote; na zaidi ya yote miujiza mikuu yote ambayo Mungu alitufanyia hata tuna viungo vyote kamili leo hii au tunahesabu mabaya tu yanayotukuta pale tunapokosa kazi, pesa, kushindwa kujenga nyumba, kutotambulika na jamii, kuugua au kudharauliwa?
1 Thesalonike 5:18

Ukuu wa Mungu katika maisha yetu hautakiwi kupimwa kwa kutizama vile vinavyoonekana zaidi kwani hivyo ni vya kitambo tu, bali vile visivyoonekana zaidi, ndio maana Neno la Mungu linatukumbusha kutamani sana karama za rohoni, zaidi pia tukipanda katika mwili tutavuna uharibifu kwani mwili ni mavumbi na udongoni utarudi.
Mathayo 6:19 – 21

Kama ambavyo Mungu alianza kuumba roho kwanza, ikampendeza hata akamuumba mwanadamu kutoka katika mavumbi; hakika mafanikio yote ya kudumu pia yenye kibali toka kwa Mungu huanza katika roho kwanza ndipo hata yaonekane katika mwili vinginevyo ni sawa na kujilisha upepo chini ya jua.
3 Yohana 1:2

Tusipokuwa na Mungu karibu na kuzingumza naye katika maombi, ni jinsi gani basi tutaweza kujua yale anayotuwazia siku zote nakutambua makuu ambayo ameshayafanya kwa ajili yetu? Sidhani kama mwajiri wako anaweza kukupandisha katika cheo usichostahili, au mzazi wako akakupa urithi ambao sio wako. Lakini ukichukua muda wa kuwa naye karibu na kuzungumza naye hakika utajua wapi umekosea ujirekebishe