Wapendwa wengi haitupi shida kuamini bila mashaka kwamba
Mungu anaweza kutenda yote, na wala hakuna gumu linalomshinda kwakuwa tunaona
mengi makuu aliyofanya pia anayoendelea kufanya Mungu kwa wengine, lakini sisi
tunaona kwamba jambo kama hilo kutimia kwetu ni ngumu zaidi.
Muujiza siku zote ni kwa mwanadamu, lakini kwa Mungu sio
muujiza kwani kwake yeye ni jambo la kutamka tu na inakuwa. Yamkini kuna
miujiza mingi sana ambayo Mungu anatutendea katika maisha yetu ila tu huwa
hatujaribu kutafakari na kumuuliza Mungu tukajua yale yaliyo sirini.
Jeremia 33:3
Dada mmoja alichelewa kuamka kwenda kazini, ingawa anaweka
kengele ya kumuamsha siku zote lakini hauisikia, hata ilipofika mchana chakula
chake kilicheleweshwa sana, zaidi aliporudi nyumbani akajaribu kupumzika na
kuweka miguu yake kwenye kifaa cha kukanda miguu ambacho hakikufanya kazi. Huyu
dada alihuzunika sana akimuuliza Mungu kwanini kila kitu hakijaenda sawa siku
hiyo. Mungu akamwambia alimsababisha achelewe kazini kwa sababu kulikuwa na
dereva mlevi njiani ambaye angemsababishia ajali pengine kupoteza maisha, pia
chakula kilichelewa kwakuwa aliyekiandaa mwanzo alikuwa anaumwa ugonjwa wa
kuambukiza na mwisho, ile mashine ya kukanda miguu ilikuwa na tatizo ambalo
lingesababisha nyumba yote ikose umeme.
Tukirejea
kwa wana wa Israel ambao Mungu alikuwa nao akiwaongoza kutoka utumwani Misri
ambako Alifanya mambo makubwa sana kwa namna tofauti hata Farao akawaachia
huru, lakini zaidi sana aliwavusha bahari ya Sham, akawalisha mana na kwele
jangwani, ila kutokana na kusahau kwao na ukaidi, Mungu anamwambia Musa kwamba
watu hawa wana shingo ngumu.
Kutoka 32:9
Wote
tunafahamu kuhusu ajali hasa za magari ambazo huwa zinatokea, kiasi kwamba
ukiona gari lilivyo unasema hakika hapa hakuna mtu aliyetoka mzima ila kwa
mshangao wetu tunaambia kwamba wote waliokuwemo wametoka wazima wakiwa na
michubuko tu.
Mbali ya
kwamba Mungu ana makusudi kwa kila jambo, hakika ukifikia viwango vya kupata
baraka utazipata tu haijalishi unazitaka au huzitaki, vivyo hivyo ukifikia
viwango vya kupata muujiza utaupata tu bila kujali unauhitaji au lah.
Isaya 43:26
Tumesahau
kuna wangapi wamekufa wakiwa watoto wadogo kabisa, au hatujaona ukuu wa Mungu
tuko hai hata leo sio wagonjwa wala kuwa na ulemavu wowote; na zaidi ya yote
miujiza mikuu yote ambayo Mungu alitufanyia hata tuna viungo vyote kamili leo
hii au tunahesabu mabaya tu yanayotukuta pale tunapokosa kazi, pesa, kushindwa
kujenga nyumba, kutotambulika na jamii, kuugua au kudharauliwa?
1 Thesalonike 5:18
Ukuu wa
Mungu katika maisha yetu hautakiwi kupimwa kwa kutizama vile vinavyoonekana
zaidi kwani hivyo ni vya kitambo tu, bali vile visivyoonekana zaidi, ndio maana
Neno la Mungu linatukumbusha kutamani sana karama za rohoni, zaidi pia
tukipanda katika mwili tutavuna uharibifu kwani mwili ni mavumbi na udongoni
utarudi.
Mathayo 6:19 – 21
Kama ambavyo
Mungu alianza kuumba roho kwanza, ikampendeza hata akamuumba mwanadamu kutoka
katika mavumbi; hakika mafanikio yote ya kudumu pia yenye kibali toka kwa Mungu
huanza katika roho kwanza ndipo hata yaonekane katika mwili vinginevyo ni sawa
na kujilisha upepo chini ya jua.
3 Yohana 1:2
Tusipokuwa na Mungu karibu na kuzingumza naye katika maombi, ni jinsi gani basi tutaweza kujua yale anayotuwazia siku zote nakutambua makuu ambayo ameshayafanya kwa ajili yetu? Sidhani kama mwajiri wako anaweza kukupandisha katika cheo usichostahili, au mzazi wako akakupa urithi ambao sio wako. Lakini ukichukua muda wa kuwa naye karibu na kuzungumza naye hakika utajua wapi umekosea ujirekebishe
No comments:
Post a Comment