Wengi wetu tumekutana na matukio mengi sana kwenye maisha
yetu ambapo tulitegemea Mungu kufanya kitu na kubadilisha mazingira kuwa vile
tunavyotaka, yamkini uliomba sana kwa ajili ya jambo fulani, au ulifanya
jitihana na kuenenda katika haki siku zote bila mafanikio hata kuona kuwa Mungu
hajibu au hakutendei haki.
Mathayo 6:10
Siku zote
mapenzi ya Mungu ndiyo huwa yanatimia katika maisha yetu. Mungu ndiye
anayepanga maisha yetu, kwakuwa anatutakia mema siku zote. Kile ambacho sisi tunakiona
kuwa ni kizuri lakini tusikipate, hakika mwisho wake ungetupeleka pabaya ndiyo
maana Mungu ametuepusha mapema.
Ndio maana maandiko yanasema kuna njia inayoonekana njema
machoni pa binadamu ila mwisho wake ni uharibifu au mauti.
Lakini,
inakuwaje kwa ndugu zetu ambao waliugua na kufa mapema? Mabaya huwapata waovu
na wema pia. Hatuwezi kuelewa kwanini mtoto anazaliwa kilema au baada ya
kuzaliwa tu anakufa, au mtu mwema akapoteza maisha kwenye ajali ambayo
haikumhusu. Tunaweza kuwaza kuwa yamkini Mungu hajatutendea haki kwa namna fulani,
ila hakika Mungu ndiye anayepanga mwanzo na mwisho wa maisha ya mwanadamu, Yeye
anaufahamu mwanzo wetu kutokea mwisho.
Katika mapigo
na mateso yote, Ayubu hakumkufuru Mungu. Pia Daudi alipopata taarifa kuwa kijana wake amekufa
aliacha kuomboleza akaoga, akavaa vema na kuelekea hekaluni kumuabudu Mungu.
Matendo 7:57 – 60 | Mathayo 14:6 – 12
Stefano alikuwa mtumishi wa Mungu lakini alipigwa mawe hata
kufa, si kwamba Mungu hakutaka au hakuweza kumuokoa, ila Mungu aliachia hilo
kwa kusudi lake mwenyewe. Pia Yohana mbatizaji, alikatwa kichwa alipokuwa
gerezani, lakini sio kwamba Mungu alishindwa kumuokoa, ila mapenzi ya Mungu
ndiyo siku zote yatatimia.
1 Thesalonike 5:16 – 18
Siku zote
inabidi turudishe sifa na shukrani kwa Mungu, kwa kila jambo linalotutokea
tukijua kwamba tumeenenda katika haki na kweli yote. Inatupasa siku zote
kufahamu kuwa kuna mambo ambayo pengine Mungu akitufunulia hatuwezi kuelewa,
lakini zaidi yatatufanya tuwe na wakati mgumu zaidi kuliko hali tuliyokuwanayo
mwanzo.
Kumbukumbu la Torati
29:29
Tunapokaa na
kushikilia sana mambo ambayo hayakufanikiwa jinsi ambavyo tungependa au
tungetaka inasababisha tukaishi maisha yetu kwa uchungu na kujilaumu au kulaumu
wengine, lakini zaidi sana inatupelekea kukosa mazuri ambayo Mungu ameandaa kwa
ajili yetu.
Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu anapoachilia baraka zije kwetu, kama hatujajiweka tayari kwenye nafasi ya kuzipokea zitatupita, na pengine tusizipate tena ambapo itatufanya kuendelea kulaumu tu siku zote.
No comments:
Post a Comment