Matunda mengi sana yanayoliwa hata yale yasiyoliwa yana
mbegu moja au Zaidi ndani yake, na mbegu hizo zinaendeleza kizazi cha hilo
tunda au muendelezo wa kuwepo kwa tunda kwa kadri maisha yanavyoendelea.
Mafanikio ya mbegu yoyote ni kuchipua ardhini hata ikawa
mmea au mti uliokomaa na kuzaa matunda mazuri yatakayoiva, lakini mbegu
isipofanikiwa kuchipua mti imeshindwa katika yote hivyo pia ilikuwa haifai
maana kusudi lake hasa halijatimia.
Katika safari
yetu ya kuelekea mbinguni haiwezekani kutenda mema na kumpendeza Mungu, zaidi
sana kuwa watakatifu kama Yeye alivyo mtakatifu kama hatutakufa kwanza halafu
tukafufuka, yaani ule utu wetu wa kale ambao unaambatana na tabia zote za asili
hautazikwa ili tufufuke tukiwa viumbe wapya.
Yohana 3:3 – 7
Siku zote za
maisha yetu inatupasa kujichunguza sana ili tujue pia kukubari mapungufu ndani
yetu, yamkini tabia za asili bado zinatutawala. Mbegu inapofukiwa ardhini huwa
inakufa kwanza hata iweze kuchipua upya. Unapoitizama mbegu iliyokufa (sio
kuoza), lile ganda lake linakuwa limechoka na kuchakaa hata kushindwa kuzuia
kile cha ndani yake kuchukua nafasi kutoka nje.
Miili yetu
inapoachwa ikachakaa na kuchoka kabisa (kutokuhisi chochote kile cha dunia hii
katika mwili wa nyama) ndipo pale tunapompa nafasi Roho wa Mungu akatawale na
kutuongoza katika mema yote.
2 Wakorintho 5:17
Ipo mimea
ambayo inadumaa, ama imechipua vema ila haizai matunda siku zote kiasi kwamba
hatuipendi kwakuwa haina faida yoyote kwetu zaidi ya kuwa mmea au mti tu lakini
kusudi lake hasa halijatimia, ndio maana tunapojichunguza inawezekana kabisa
tumechipua lakini hatukui, au tunakua lakini hatuzai matunda wala hakuna dalili
ya kuzaa matunda kwa sababu utu wetu wa kale bado umo ndani yetu, ama yamkini
bado tunaipenda dunia kwa kiasi Fulani, na hatujataka kuiacha miili yetu ya
nyama kufa kabisa.
Yohana 15:1 – 8
Siku zote mbegu inayopandwa katika udongo mzuri huzaa sana,
vivyo hivyo nasi inatupasa tujiweke kwenye mazingira mazuri ya kukua kiroho,
kuondokana na vishawishi vya tamaa na tabia za dunia hii kuchukua nafasi tena
katika maisha yetu hata tukarudi nyuma kabisa ama kuwa vuguvugu.
Tunapokuwa
kwenye mazingira sahihi ya kiroho na kimwili hakika tunauona utukufu wa Mungu
ukituzunguka muda wote na kutawala maisha yetu, maana Mungu huwa hatuachi bali
dhambi zetu wenyewe zinatutenganisha na uwepo wa Mungu, kama ambavyo mbegu iko
tayari kufa ili ichipue tena na kuzaa lakini kuiteketeza mbegu ni kuiweka
katika mazingira yasiyofaa.
Isaya
59:2
No comments:
Post a Comment