Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Friday, June 28, 2013

Kuitambua Njia

Ni rahisi sana kujua njia inakutoa wapi na kukupeleka wapi, lakini inahitajika kazi ya ziada na umakini wa kutosha kutambua misukosuko iliyopo njiani. Dereva yeyote mzuri, anapopita njia kwa mara ya kwanza anakuwa makini sana, tofauti na anavyopita mara ya pili au zaidi maana tayari anajua hatari au vikwazo viko wapi, yaani amekuwa mzoefu.

Wana wa Israeli walitumia miaka 40 jangwani wakisafiri toka Misri kwenda Caanan katika njia ambayo iliwapasa kutumia siku 40 tu. Nataka kuamini kuwa umbali wa safari yao waliujua ila tu kwakuwa hawakujipanga kukabiliana na misukosuko pamoja na hatari zote wakimtumaini Mungu, ndio maana iliwangarimu miaka 40 badala ya siku 40 kwakuwa walikuwa wakilaumu na kulalamika katika kila ambacho walikosa.
Kutoka 16:2 – 3 | Hesabu 11:1 | Hesabu 14:1 – 4

Tofauti sana na Yusufu ambaye sio tu kufahamu, lakini pia alitambua njia aliyokuwa akiiendea, ndio maana tunamuona Yusufu akikataa kujihusisha kwenye uzinzi na mke wa Potifa. Yusufu aliamini kuwa ndoto alizoota (Mwanzo 37:6 – 11) hakika itakuwa kweli, naamini pia alijua kuwa siku zote yampasa kukaa na kudumu katika mpango wa Mungu akitenda mema.

Tulipokuwa, tulipo na tunapoelekea katika maisha yetu inawezekana tulitakiwa tuwe tumeshafika lakini bado yamkini hata safari hatujaianza kwakuwa tunafanya yote katika namna na kawaida ya jamii nzima. Lakini kuna ulemavu pia, maana mjinga akimuelimisha mjinga hakuna atakaye elimika. Kifaranga wa tai anapototolewa na kuku siku zote yeye atajiona kama kuku, wala si tai ingawa atakuwa tofauti kabisa na vifaranga wengine.

Ndio maana hazina kubwa hapa ulimwenguni haiko kwenye migodi, wala si kwenye benki ya dunia wala mashamba makubwa ya wakulima ila hazina kubwa ya dunia hii iko kwenye makaburi, ambapo ndimo walipozikwa watu ambao kama wangetambua njia wanayoiendea, basi dunia yetu leo ingekuwa ni mahali pa tofauti sana. 
Makaburini kuna falsafa nyingi, ugunduzi mpya wa maboresho, taaluma nyingi ambazo Mungu aliwapa hazina hao watu lakini kwa sababu moja au nyingine wametoweka mapema kwa kupita njia isiyofaa au waliamua kuishi maisha ya watu wengine. Hakika, mzabibu usiozaa matunda mazuri haufai tena ila kukatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 7:19

Inabidi kujiuliza leo kwamba tulipoanza safari hii, tulijua tunaelekea wapi, tuliitambua njia pamoja na kujiona kuwa tayari tumefika au lah! Haiba ya Mungu ni kuuona mwisho kutokea mwanzo (Isaya 46:10) hivyo kama tunaithibitisha tabia ya Mungu ndani yetu yatupasa kuuona mwisho tukiwa mwanzo.

Waebrania 11:1
Imani iliyo kamili ni kuwa na uhakika, yaani kushikilia kitu sio kwamba tukijua kuwa kitakuwa ila kuthibitisha kuwa kimeshakuwepo, kukiongea, kukitamka na kukiishi.
Zaidi sana katika yote tunayoenenda tukipanga na kufanya haitakiwi tuwe na haraka, maana Yakobo alikuwa na haraka kuwa na mke hatimaye akapewa dada wa mhusika (Mwanzo 29:15 – 30), lakini zaidi tukijali kuukomboa wakati.
Waefeso 5:15 – 16

Kitu kimoja, ambacho pia ni hazina ya msingi sana ni muda, na kwakutokutumia muda vema wengi tunapoteza sana muda tukifanya mambo yasiyo ya msingi.

No comments:

Post a Comment