Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Wednesday, June 27, 2012

Jesus Is Coming Again

Lift up the trumpet, and loud let it ring:
Jesus is coming again!
Cheer up, ye pilgrims, be joyful and sing:
Jesus is coming again!

Refrain
Coming again, coming again,
Jesus is coming again!

Echo it, hilltops; proclaim it, ye plains:
Jesus is coming again!
Coming in glory, the Lamb that was slain;
Jesus is coming again!

Refrain

Heavings of earth, tell the vast, wondering throng:
Jesus is coming again!
Tempests and whirlwinds, the anthem prolong;
Jesus is coming again!

Refrain

Nations are angry—by this we do know
Jesus is coming again!
Knowledge increases; men run to and fro;
Jesus is coming again!

Refrain

Wednesday, June 20, 2012

Kile Kinachotushibisha



Mtu ambaye hali vyakula vyenye kuleta afya na kuulinda mwili ikiwa ni pamoja na kunywa maji kwa wingi hakika hatakuwa mwenye afya nzuri, na mara nyingi mtu huyu atasumbuliwa na magonjwa ya hapa na pale; ndio maana ukiungua daktari anasisitiza sana upate chakula bora pamoja na maji ya kutosha.

Wengi wetu tuko makini sana kuujali mwili, katika kuulisha chakula pamoja na tamaa zake, lakini tunasahau kuwa mwili ni mavumbi, na hakika mavumbini utarudi tu. Sote tunakula mara tatu kwa siku hasa kwa wengi wetu wenye maisha ya kawaida.
Mwanzo 3:19

Inatupasa kufahamu kuwa mtu wetu wa ndani (Roho) nayo pia inabidi kula na kushiba kila siku tena hata kula muda wote kwani mwili huu wa nyama hauishi milele ila roho ndiyo itakayoishi milele. Roho zetu zinahitaji kulishwa chakula sahihi ambacho ni Neno la Mungu. Kama ilivyo kawaida kuwa kile anachopanda mtu hakika ndicho anachovuna, kwani huwezi kupanda mahindi ukavuna karanga.
Wagalatia 6:7

Wengi tunapenda sana kusikiliza miziki, au kushiriki  mazungumzo ambayo hayatujengi wala kutusaidia kabisa, na pia nyakati tofauti tumekuwa tukitizama vipindi kwenye luninga ambavyo vinatujaza uovu, zaidi pia kuna magazeti mengi ambayo sisi tunaoifuata kweli hatutakiwi kujihusisha nayo kwakuwa yamkini usione ubaya wake sasa ila kadri muda unavyosonga ile mbegu iliyopandwa inakua na kuanza kuzaa matunda.
Mithali 15:14

Inatupasa tufahamu, unaposikiliza wimbo unaoelezea mtu na mwenzi wake wa zamani kwa muda, kitakachokuijia akilini ni mwezi wako wa zamani pia. Hizi tamthilia zinazoonyesha jinsi watu wasivyo waaminifu katika maisha na ndoa zao, zinapoujaza moyo wako kwa muda hakika kitakachokutokea ni wewe kukubaliana kwamba hiyo ndiyo hali ya maisha ya kuiendea na kuishi. Ukiishi kwa kusoma, kuangalia na kusikiliza mizaha hakika nawe unatakuwa na mizaha tu.
Mithali 23:7a

Katika maisha haya ya utandawazi, ambayo kila mtu ana uhuru wa kufanya chochote kile anachoona kinafaa, hata wazazi wanakosa haki ya kuwakemea watoto wao; inatupasa kukaa na kung’ang’ania katika sharia ya Mungu siku zote na muda wote. Si vema kupoteza wokovu wako wa thamani sana uliopewa bure kwa ajili ya gazeti la udaku, au tamthilia inayopita au mziki ambao unakuvutia sana kila unapousikiliza.
Wagalatia 6:8

Zaburi 119:37
Kama Daudi alivyoamua kutokujizuia kumtizama mke wa Uria alipokuwa akioga, hata ikampelekea kutenda dhambi moja baada ya nyingine; inawezekana kabisa sinema tunazozipenda, magazeti au miziki ikatupelekea kutenda dhambi mbele za Mungu. Tutambue leo na kumuomba Mungu atusaidie, zaidi tuwe watu wa kujizuia sana.

Saturday, June 16, 2012

Twende Kwa Yesu

1. Twende kwa Yesu, mimi nawe,
Njia atwonya tuijue
Imo chuoni; na mwenyewe,
Hapo asema, njoo!
Na furaha tutaiona,
Mioyo ikitakata sana,
Kwako mwokozi kuonana,
Na milele kukaa.
2. ”Wana na waje, ”atwambia.
Furahini mkisikia;
Ndiye mfalme wetu pia,
Na tumtii, njoo.
Na furaha tutaiona,
Mioyo ikitakata sana,
Kwako mwokozi kuonana,
Na milele kukaa.
3. Wangojeani? Leo yupo;
Sikiza sana asemapo;
Huruma zake zikwatapo,
Ewe kijana, njoo.
Na furaha tutaiona,
Mioyo ikitakata sana,
Kwako mwokozi kuonana,
Na milele kukaa.

Friday, June 15, 2012

Jirani Mwema



Tunapopatwa na shida, yule ambaye tunatarajia anaweza kutupa msaada au kutuokoa kutoka janga tulilonalo ni ndugu au rafiki wa karibu sana, kwanini? Kwa sababu, ndugu au rafiki wa karibu ndiye mtu pekee ambaye anaweza kuhisi uzito wa tatizo tulilonalo au magumu tunayopitia kana kwamba ni lake. Lakini katika uhalisia, ndugu au mtu wa karibu sana anaweza asikusaidie kabisa, ndio maana maandiko yanasema amelaaniwa mtu yule amtumainiaye mwanadamu.
Yeremia 17:5

Msamaria mwema! Huyu alimsaidia Myahudi aliyepigwa na wanyang’anyi akanyang’anywa kila kitu hata kuachwa nusu mfu. Katika hili tungetegemea Kuhani au Mlawi ndiye ambaye angekuwa kwenye uhalisia wa kumsaidia mtu wa taifa moja naye, lakini haikuwa hivyo maana wote wawili walitizama kando wakampita na kumuacha alivyo, wakaenda zao.
Luka 10:25 – 37

Jaribu kutafakari unapokuwa katika nchi yako mwenyewe lakini unapata shida, ndugu wa karibu pia rafiki wanashindwa kukusaidia hata anakuja mtu mgeni kabisa kutoka nchi nyingine na kukupa msaada utajisikiaje? Na huyu hasa ndio ndugu, rafiki na jirani yako. Yamkini kuna watu wameiacha Imani kwakuwa hawakupata upendo na msaada ndani ya kanisa. Dini iliyo nzuri ni ya kuwajali yatima na wajane.

Mathayo 5:43 – 48
Adui yako ambaye alikufanyia ubaya ambao yeye mwenyewe hajausahau, pia hategemei kabisa kupata masaada toka wako, siku ukamsaidia kwa gharama zote bila kumdai hakika utamfanya ajitizame na kuzidi kujuta zaidi.
Mathayo 5:20

Mtumishi mmoja wa Mungu, alielezea siku moja amepita kwenye mgahawa kununua chakula cha mchana ikatokea bahati mbaya akapenyeza gari yake mbele ya dada ambaye naye alikuwa akielekea kwenye foleni hiyo, ikasababisha yule dada kuwa mkali sana kiasi yule mtumishi akaogopa. Lakini kwakuwa alikuwa mbele yake, wakati anasubiri kupatiwa chakula chake aondoke, akamwambia mhudumu kuwa analipa pia gharama ya chakula alichoagiza yule dada nyuma yake; mhudumu akamuuliza kwani ni ndugu yako? Akamjibu hapana! Hapana! ila imenipendeza tu nimlipie. Anasema alisimamisha gari yake kwa mbali kidogo atizame hali itakayompata yule dada kuona mtu aliyemfokea sana kamlipia chakula cha mchana, pengine alikwenda kusimulia kwa siku kadhaa.
Zaburi 34:14

Jirani yetu si mwanadamu tunayemuona, kwakuwa mwanadamu yawezekana asikusaidie pale wewe unapohitaji msaada. Ni mara ngapi mahali ambapo umeweka tegemeo lako halafu hukusaidiwa kabisa? Lakini pia ni mara ngapi tumetegemewa kutoa msaada lakini tukaamua kutizama pembeni? Jirani pekee ni Yesu, ambaye ukiwa karibu naye hatakutupa wala kukuacha. Mungu huonekana akitumia watu kutusaidia katika shida na matatizo mbali mbali, lakini pia pale inapombidi Yeye ashuke hakika anashuka.

Wednesday, June 13, 2012

Mapenzi ya Mungu Yatimie



Wengi wetu tumekutana na matukio mengi sana kwenye maisha yetu ambapo tulitegemea Mungu kufanya kitu na kubadilisha mazingira kuwa vile tunavyotaka, yamkini uliomba sana kwa ajili ya jambo fulani, au ulifanya jitihana na kuenenda katika haki siku zote bila mafanikio hata kuona kuwa Mungu hajibu au hakutendei haki.

Mathayo 6:10
Siku zote mapenzi ya Mungu ndiyo huwa yanatimia katika maisha yetu. Mungu ndiye anayepanga maisha yetu, kwakuwa anatutakia mema siku zote. Kile ambacho sisi tunakiona kuwa ni kizuri lakini tusikipate, hakika mwisho wake ungetupeleka pabaya ndiyo maana Mungu ametuepusha mapema.
Ndio maana maandiko yanasema kuna njia inayoonekana njema machoni pa binadamu ila mwisho wake ni uharibifu au mauti.

Lakini, inakuwaje kwa ndugu zetu ambao waliugua na kufa mapema? Mabaya huwapata waovu na wema pia. Hatuwezi kuelewa kwanini mtoto anazaliwa kilema au baada ya kuzaliwa tu anakufa, au mtu mwema akapoteza maisha kwenye ajali ambayo haikumhusu. Tunaweza kuwaza kuwa yamkini Mungu hajatutendea haki kwa namna fulani, ila hakika Mungu ndiye anayepanga mwanzo na mwisho wa maisha ya mwanadamu, Yeye anaufahamu mwanzo wetu kutokea mwisho.
Katika mapigo na mateso yote, Ayubu hakumkufuru Mungu. Pia Daudi  alipopata taarifa kuwa kijana wake amekufa aliacha kuomboleza akaoga, akavaa vema na kuelekea hekaluni kumuabudu Mungu.

Matendo 7:57 – 60 | Mathayo 14:6 – 12
Stefano alikuwa mtumishi wa Mungu lakini alipigwa mawe hata kufa, si kwamba Mungu hakutaka au hakuweza kumuokoa, ila Mungu aliachia hilo kwa kusudi lake mwenyewe. Pia Yohana mbatizaji, alikatwa kichwa alipokuwa gerezani, lakini sio kwamba Mungu alishindwa kumuokoa, ila mapenzi ya Mungu ndiyo siku zote yatatimia.

1 Thesalonike 5:16 – 18
Siku zote inabidi turudishe sifa na shukrani kwa Mungu, kwa kila jambo linalotutokea tukijua kwamba tumeenenda katika haki na kweli yote. Inatupasa siku zote kufahamu kuwa kuna mambo ambayo pengine Mungu akitufunulia hatuwezi kuelewa, lakini zaidi yatatufanya tuwe na wakati mgumu zaidi kuliko hali tuliyokuwanayo mwanzo.
Kumbukumbu la Torati 29:29

Tunapokaa na kushikilia sana mambo ambayo hayakufanikiwa jinsi ambavyo tungependa au tungetaka inasababisha tukaishi maisha yetu kwa uchungu na kujilaumu au kulaumu wengine, lakini zaidi sana inatupelekea kukosa mazuri ambayo Mungu ameandaa kwa ajili yetu.
Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu anapoachilia baraka zije kwetu, kama hatujajiweka tayari kwenye nafasi ya kuzipokea zitatupita, na pengine tusizipate tena ambapo itatufanya kuendelea kulaumu tu siku zote.

Thursday, June 7, 2012

Yeye Mwenye Majibu Ya Yote


Nchi zilizoendelea, kuna matajiri wenye magonjwa ambayo bado madaktari hawajapata tiba wala suluhisho lake hivyo wanalipa pesa nyingi sana ili kugandisha miili yao, hivyo warudishwe kwenye uhai pale tiba itakapopatikana ili waweze kuishi muda mrefu zaidi.

Miaka ya nyuma, iliwezekana kulala bila kufunga milango kwa makomeo, pia watu walipaki magari yao nje bila kuyafunga hata ilipofika asubuhi hakukuwa na wizi wowote, lakini maisha ya leo tunafunga milango nyuma ya milango ya chuma na kuweka ulinzi wote, pamoja na uzio wa umeme lakini bado hatuko salama.

Mithali 14:12
Siku zote suluhisho la mwanadamu katika tatizo moja, kama hajaongozwa na Mungu hakika linatengeneza tatizo jingine kubwa zaidi hapo baadaye. Magari yanaturahisishia sana usafiri kila siku lakini pia ndicho chombo kinachosababisha ajali mbaya kila siku. Pombe ilitengenezwa kama sehemu ya starehe lakini ndio chanzo cha magonjwa sugu yasiyo na tiba hata sasa. Simu za mkononi zinaturahisishia sana kuwasiliana lakini ndio chanzo cha maovu mengi na ndoa kuvunjika.

Mithali 3:5 – 6
Mungu hakika ndiye muweza wa yote, yeye anaifahamu mipaka ya dunia, Yeye ndiye anayesimamisha falme na kuziangusha, Yeye ndiye anayetoa kibali kwa kila jambo, pia ni Yeye anayeijua sekunde inayofuata hata kesho na milele yote, Yeye anajua milele ina umbali wa kiasi gani, Yeye anauona mwanzo kutokea mwisho, Yeye anatujua kabla hata mimba hazijatungwa kwenye matumbo ya mama zetu, Yeye ni yule yule milele yote habadiriki. Unapojaribu kufanya mambo kwa ufahamu na njia zako hakika wewe umepotea.
1 wakorintho 1:25

Watafiti wanavumbua mambo mengi sana yanayoonekana mazuri, watu wanapata utajiri kutokana na jitihada zao katika maisha na mafanikio pia yanaonekana lakini kama sio mpango wa Mungu katika yote daima huwa ni ubatili tu, sawa na kujilisha upepo chini ya jua.
Solomon katika fahari yake alikuwa tajiri sana, alikuwa na mali kuliko mwanadamu yeyote aliyewahi kuishi, alioa wake 700 na akawa na Masuria 300 lakini mwisho alifahamu kuwa yote ni ubatili mtupu.
1 Wafalme 11:3 | Mhubiri 1:1 – 10

Jibu la Ukimwi analo Mungu, Jibu la kuvunjika kwa ndoa analo Mungu, Jibu la ugonjwa wa Kisukari, Kansa na Shinikizo la damu pia analo Mungu, Jibu la kuyumba kwa uchumi analo Mungu, Jibu la kuongezeka kwa maasi na vita analo Mungu, Jibu la utoaji mimba pia hakika ni Mungu pekee aliyenalo.
Ufunuo 3:17 – 19

Ukimtumainia mwanadamu leo atakusaidia bali kesho atakukimbia, yamkini atakushauri lililo jema leo lakini yawezekana kesho atakupotosha, maana binadamu tunabadirika ndio maana amelaaniwa mtu yule amtumainiaye mwanadamu. Lakini Mungu tu ndiye habadiriki, Naye atakupa jibu sahihi.

Friday, June 1, 2012

Ukikubali na Kutii



Ukubali na utiifu wetu kwenye sheria, amri na Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha yetu ya wokovu, na zaidi sana ili kuweza kusonga mbele tukimuona Mungu akitujenga upya na kufanya yaliyo makuu sana kupitia sisi.

Katika hali ya kawaida sana kwa kila binadamu, inakuwa rahisi sana kutii ila si kukubali, maana unatii ile mamlaka kutokana na hofu hivyo ukatekeleza ila ndani yako hujakubaliana na hilo jambo. Lakini kukubali kunakuwepo kutokana na Imani ndani yako, hasa Imani iliyo timilifu.

Isaya 1:19 Ukikubali na kutii utakula mema ya nchi….
Sheria ya Mungu ni nzuri sana kwani ipo ili kutulinda pamoja na kutuepusha na mabaya siku zote za maisha yetu. Mungu alipowaambia Adam na Eva wasile tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya alitaka kuthibitisha kwamba wanamtii, lakini zaidi ya yote endapo wamekubaliana na kile anachokisema.
Mwanzo 2:16 – 17
Viumbe wanaoishi kwenye maji wamekubali  na wanatii sheria waliowekewa na Mungu, pia ndege wa angani hata wadudu na wanyama wa porini, ndio maana siku zote wanaishi bila shida. Lakini sisi binadamu ambao tuliumbwa kwa kwa mfano wa Mungu siku zote tunajaribu kuhakiki uhalisia wa kile ambacho Mungu amekisema.

Mathayo 6:31 – 34
Matatizo mengi katika maisha siku hizi ni kwasababu kila mtu anataka kuwa yeye na mahitaji yake, au kile ambacho yeye hasa anataka kukifanya. Ni kutokana na mahangaiko pamoja na msongo wa mawazo katika kizazi hiki tunaongezeko kubwa sana la magonjwa ya kansa, shinikizo la damu na kisukari. Hii ni kwakuwa hatutaki kutii na kukubaliana na ukweli kwamba kesho tumuachie Mungu, lakini pia ni jukumu letu kuutafuta ufalme wake kwanza na haki yake.
Bila Imani inakuwa ngumu sana kukubali, kwani pale unapomuamini mtu ndipo unapoweza kukubaliana naye. Usipomwamini mwajiri wako huwezi kuendelea kumtumikia, zaidi usipomuamini mwenzi wako inakuwa ni ngumu kuishi naye pamoja.
Panapokosekana Imani kunajengeka mashaka na woga ambao hutoka kwa Shetani. Ili kumuona Mungu katika uhalisia wake maishani mwetu lazima tuwe na Imani timilifu maana haiwezekani kumpendeza Yeye pasipo Imani.
2 Timotheo 2:11 – 13

Mtu mwenye utii na kukubali siku zote hubarikiwa, na katika mambo yake siku zote atafanikiwa na kuwa juu ya mataifa.
Kumbukumbu la Torati 28:1 - 14