Tunapopatwa
na shida, yule ambaye tunatarajia anaweza kutupa msaada au kutuokoa kutoka
janga tulilonalo ni ndugu au rafiki wa karibu sana, kwanini? Kwa sababu, ndugu au
rafiki wa karibu ndiye mtu pekee ambaye anaweza kuhisi uzito wa tatizo tulilonalo
au magumu tunayopitia kana kwamba ni lake. Lakini katika uhalisia, ndugu au mtu
wa karibu sana anaweza asikusaidie kabisa, ndio maana maandiko yanasema
amelaaniwa mtu yule amtumainiaye mwanadamu.
Yeremia 17:5
Msamaria mwema! Huyu alimsaidia Myahudi aliyepigwa na wanyang’anyi
akanyang’anywa kila kitu hata kuachwa nusu mfu. Katika hili tungetegemea Kuhani
au Mlawi ndiye ambaye angekuwa kwenye uhalisia wa kumsaidia mtu wa taifa moja naye,
lakini haikuwa hivyo maana wote wawili walitizama kando wakampita na kumuacha
alivyo, wakaenda zao.
Luka 10:25 – 37
Jaribu kutafakari unapokuwa
katika nchi yako mwenyewe lakini unapata shida, ndugu wa karibu pia rafiki
wanashindwa kukusaidia hata anakuja mtu mgeni kabisa kutoka nchi nyingine na
kukupa msaada utajisikiaje? Na huyu hasa ndio ndugu, rafiki na jirani yako.
Yamkini kuna watu wameiacha Imani kwakuwa hawakupata upendo na msaada ndani ya
kanisa. Dini iliyo nzuri ni ya kuwajali yatima na wajane.
Mathayo 5:43 – 48
Adui yako ambaye alikufanyia ubaya ambao yeye mwenyewe hajausahau, pia
hategemei kabisa kupata masaada toka wako, siku ukamsaidia kwa gharama zote
bila kumdai hakika utamfanya ajitizame na kuzidi kujuta zaidi.
Mathayo 5:20
Mtumishi mmoja wa Mungu, alielezea siku moja amepita kwenye mgahawa kununua
chakula cha mchana ikatokea bahati mbaya akapenyeza gari yake mbele ya dada
ambaye naye alikuwa akielekea kwenye foleni hiyo, ikasababisha yule dada kuwa
mkali sana kiasi yule mtumishi akaogopa. Lakini kwakuwa alikuwa mbele yake,
wakati anasubiri kupatiwa chakula chake aondoke, akamwambia mhudumu kuwa
analipa pia gharama ya chakula alichoagiza yule dada nyuma yake; mhudumu
akamuuliza kwani ni ndugu yako? Akamjibu hapana! Hapana! ila imenipendeza tu
nimlipie. Anasema alisimamisha gari yake kwa mbali kidogo atizame hali
itakayompata yule dada kuona mtu aliyemfokea sana kamlipia chakula cha mchana,
pengine alikwenda kusimulia kwa siku kadhaa.
Zaburi 34:14
Jirani yetu si mwanadamu
tunayemuona, kwakuwa mwanadamu yawezekana asikusaidie pale wewe unapohitaji
msaada. Ni mara ngapi mahali ambapo umeweka tegemeo lako halafu hukusaidiwa
kabisa? Lakini pia ni mara ngapi tumetegemewa kutoa msaada lakini tukaamua
kutizama pembeni? Jirani pekee ni Yesu, ambaye ukiwa karibu naye hatakutupa
wala kukuacha. Mungu huonekana akitumia watu
kutusaidia katika shida na matatizo mbali mbali, lakini pia pale inapombidi Yeye
ashuke hakika anashuka.
No comments:
Post a Comment