Kuiona siku nyingine mpya ni upendeleo, zaidi ni baraka ya
pekee sana kutoka kwa Mungu wetu ingawa kwa wengi wetu hatujui uthamani wa kuiona
tena siku nyingine ila inakuwa ni kawaida tu au mazoea yasiyobeba uzito wowote.
Mungu wetu ametujalia
furaha ya kuwa nayo siku zote na wakati wote, ingawa muda mwingi na katika
mambo mengi tunachagua kuwa na hofu tukihuzunika sana. Jambo moja la msingi
kukumbuka siku zote ni kwamba kinachotutenganisha sisi na furaha ni kutokulijua
Neno la Mungu, maana Neno linatuambia wazi majonzi hudumu usiku lakini furaha
huja asubuhi.
Zaburi 30:5
KInachotuumiza
ni kwakuwa tunaamua kuhangaikia sana vile ambayo havitakiwi kuhangaikiwa, pia
hatujui namna ya kuthamanisha vile tulivyonavyo tukishukuru na kumtukuza Mungu,
ndio maana siku zote tunajiona sisi ni wahitaji tu, zaidi haijawahi kufikia
siku tukatosheka.
Mathayo 6:25 – 34
| 1 Timotheo 6:6 – 10
Wengi tunajawa na hasira pamoja na uchungu kutokana na
matukio mbali mbali yanayotukuta kwenye maisha yetu ya kila siku, pia hatuwezi
kuizuia hasira kutufika wala uchungu lakini hatutakiwi kuviruhusu vitutawale
maishani mwetu. Hata kwenye msiba wanaomboleza kwa muda, lakini wakiendelea
kuomboleza siku zote ina maana wameamua kubadili mfumo wa maisha Mungu
aliouweka kabisa. Tunapoishi kwa maumivu ya jana au siku za nyuma ina maana
tumeamua kuikataa leo.
Zaburi 118:24
Mtumishi wa Mungu Daudi alilitambua kwamba kila siku ni
mpya, na inampasa kushangilia na kushukuru katika hiyo. Nasi inatupasa kubadili
namna ya maisha yetu, tukubali kwa yote yaliyopita hakika hatuwezi
kuyabadilisha ila tunaweza kuanza sasa na kufanya yaliyo mema zaidi mbele za
Mungu na jirani zetu.
Tunapoikataa
furaha asubuhi tunampa shetani nafasi kuiteka siku yetu, ndio maana kuna watu
wanasema wameamka vibaya ingawa hawaumwi ila anakuwa na hasira tu siku nzima
wala hajisikii kufanya kitu chochote. Cha msingi cha kufahamu ni kwamba furaha
ni chaguo kama ambavyo huzuni pia ni chaguo la mtu binafsi. Ndio maana Joshua
aliwaambia wana wa Israeli wachague ni nani watakayemtumikia ila yeye na nyumba
yake wanamtumikia Bwana.
Joshua 24:15
Tunapoamka asubuhi tunatizama nini? Tunakumbuka jana ilikuwa
mbaya kiasi gani, tunatizama ni vingapi ambavyo tunahitaji lakini hatuna au
tunatizama jinsi ambavyo hatuko kama wengine? Haya yote tunapoyatizama
yanatuletea huzuni siku nzima, lakini tukiangalia uhalisia wa kwamba ni siku
nyingine mpya, tukamshukuru Mungu kwa uzima na afya njema, tukaona taswira ya
Mungu ndani yetu, na kujua kuwa Mungu yupo kazini kutubariki, kututetea, kutupigania
na kutuongoza; hakika hatutakuwa na muda wa kuikumbatia huzuni na hasira.
Furaha ni hali inayokosekana kwa watu wengi sana, hata
tunakosa amani moyoni pengine hata kukata tamaa ya maisha kabisa. Siri moja ya
msingi, inatakiwa tufurahie kwanza vile tulivyonavyo, zaidi sana jinsi tulivyo
ndipo tutasababisha Mungu atubariki kwa vingine vingi zaidi.
No comments:
Post a Comment