Maisha yetu kwa sehemu kubwa sana yamejawa na mtazamo wa
kutizama ni kipi ambacho hatuna, ama ni wapi ambapo tunahangaika daima. Hakika
duniani tunayo dhiki, lakini katika uhalisia tumebarikiwa sana kuliko dhiki
tulizonazo, zaidi sana dhiki yetu ni ya kitambo kifupi tu.
Tunapohesabu baraka, tunaruhusu ukuu na uweza wa Mungu
uonekane katika maisha yetu siku zote, zaidi tunaweza kuona na kujua kuwa Mungu
yuko kazini akijishughulisha kwa ajili ya mambo yetu kuliko ambavyo tunaweza
kutafakari na kuona.
Zaburi 100:4
Ukimtizama mtoto mdogo, anajua kuwa kila kitu kipo, tena
anajua kuwa baba ana pesa ya kutosha kumnunulia kila anachohitaji, ndio maana
siku zote watoto wana furaha na amani. Lakini pia watoto hawajui kupima uzito
wa mahitaji muhimu, hivyo hatutakiwi kuwa kama watoto katika hili bali
tutafakari siku zote mema ambayo Mungu ametufanyia na kushukuru tukimsifu
daima.
Kubarikiwa
si kuwa na majumba ya kifahari, wala magari na pesa nyingi bali kuwa mzima
mwenye afya tele pamoja na amani ipitilizayo amani zote tukipata kibali kila
tuendapo. Kubarikiwa pia ni kumjua sana Mungu tukizishika amri zake.
Ayubu 22:21
Mtu anapobarikiwa na Mungu, anatosheka anakuwa hana uhitaji
tena, ndio maana Bwana Yesu alimwambia yule mwanamke Msamaria kuwa akinywa maji
atakayompa Yeye hakika hataona kiu tena. Kitu chochote kile kilichobarikiwa na
Mungu kinatosha kabisa wala hakihitaji nyongeza. Lakini tunapokuwa na mali ama
utajiri ila tunahitaji kupata zaidi inabidi tujikague na kumuuliza Mungu kuwa
ni baraka toka kwake au lah, kwa maana wengi wameacha kumuabudu Mungu wakaabudu
mali na utajiri.
Yakobo 3:10
Mungu ametupa uwezo wa kujitamkia na kuwatamkia wengine
laana au baraka, lakini mara nyingi tunatumia ndimi wetu kulaani badala ya
kubariki. Mara nyingi tunajiambia kwamba hii kazi ikiisha sijui itakuwaje, ama
siwezi kufanya biashara, au mke wangu ni mkorofi sana, ama watoto wangu ni
wakaidi mno, au sidhani kama nitafanikiwa daima pamoja na mengine mengi. Haya
pia huwa tunayazungumza kwa wengine hata tukawalaani.
Warumi 12:2
Kwa Mungu
wetu hakuna laana, wala magomvi yoyote bali kuna amani, upendo, upole pamoja na
baraka tele. Mataifa huenenda wakitizama nini au kipi wanakosa na wapi
wamepungukiwa wakizidi kuona kwamba hakika maisha hayawatendei haki, bali sisi
si wa dunia tena na haitupasi kuenenda kama wao.
Wafilipi 4:8
Inatupasa kutambua baraka zetu kama jinsi ambavyo zinatuzunguka, lakini pia inatubidi kukiri baraka hata kabla hatujaziona kwa macho ya nyama, cha msingi tumeshamuomba MUngu na kuamini hakika itakuwa sawa sawa na kuamini kwetu.
No comments:
Post a Comment