Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Friday, June 28, 2013

Kuitambua Njia

Ni rahisi sana kujua njia inakutoa wapi na kukupeleka wapi, lakini inahitajika kazi ya ziada na umakini wa kutosha kutambua misukosuko iliyopo njiani. Dereva yeyote mzuri, anapopita njia kwa mara ya kwanza anakuwa makini sana, tofauti na anavyopita mara ya pili au zaidi maana tayari anajua hatari au vikwazo viko wapi, yaani amekuwa mzoefu.

Wana wa Israeli walitumia miaka 40 jangwani wakisafiri toka Misri kwenda Caanan katika njia ambayo iliwapasa kutumia siku 40 tu. Nataka kuamini kuwa umbali wa safari yao waliujua ila tu kwakuwa hawakujipanga kukabiliana na misukosuko pamoja na hatari zote wakimtumaini Mungu, ndio maana iliwangarimu miaka 40 badala ya siku 40 kwakuwa walikuwa wakilaumu na kulalamika katika kila ambacho walikosa.
Kutoka 16:2 – 3 | Hesabu 11:1 | Hesabu 14:1 – 4

Tofauti sana na Yusufu ambaye sio tu kufahamu, lakini pia alitambua njia aliyokuwa akiiendea, ndio maana tunamuona Yusufu akikataa kujihusisha kwenye uzinzi na mke wa Potifa. Yusufu aliamini kuwa ndoto alizoota (Mwanzo 37:6 – 11) hakika itakuwa kweli, naamini pia alijua kuwa siku zote yampasa kukaa na kudumu katika mpango wa Mungu akitenda mema.

Tulipokuwa, tulipo na tunapoelekea katika maisha yetu inawezekana tulitakiwa tuwe tumeshafika lakini bado yamkini hata safari hatujaianza kwakuwa tunafanya yote katika namna na kawaida ya jamii nzima. Lakini kuna ulemavu pia, maana mjinga akimuelimisha mjinga hakuna atakaye elimika. Kifaranga wa tai anapototolewa na kuku siku zote yeye atajiona kama kuku, wala si tai ingawa atakuwa tofauti kabisa na vifaranga wengine.

Ndio maana hazina kubwa hapa ulimwenguni haiko kwenye migodi, wala si kwenye benki ya dunia wala mashamba makubwa ya wakulima ila hazina kubwa ya dunia hii iko kwenye makaburi, ambapo ndimo walipozikwa watu ambao kama wangetambua njia wanayoiendea, basi dunia yetu leo ingekuwa ni mahali pa tofauti sana. 
Makaburini kuna falsafa nyingi, ugunduzi mpya wa maboresho, taaluma nyingi ambazo Mungu aliwapa hazina hao watu lakini kwa sababu moja au nyingine wametoweka mapema kwa kupita njia isiyofaa au waliamua kuishi maisha ya watu wengine. Hakika, mzabibu usiozaa matunda mazuri haufai tena ila kukatwa na kutupwa motoni.
Mathayo 7:19

Inabidi kujiuliza leo kwamba tulipoanza safari hii, tulijua tunaelekea wapi, tuliitambua njia pamoja na kujiona kuwa tayari tumefika au lah! Haiba ya Mungu ni kuuona mwisho kutokea mwanzo (Isaya 46:10) hivyo kama tunaithibitisha tabia ya Mungu ndani yetu yatupasa kuuona mwisho tukiwa mwanzo.

Waebrania 11:1
Imani iliyo kamili ni kuwa na uhakika, yaani kushikilia kitu sio kwamba tukijua kuwa kitakuwa ila kuthibitisha kuwa kimeshakuwepo, kukiongea, kukitamka na kukiishi.
Zaidi sana katika yote tunayoenenda tukipanga na kufanya haitakiwi tuwe na haraka, maana Yakobo alikuwa na haraka kuwa na mke hatimaye akapewa dada wa mhusika (Mwanzo 29:15 – 30), lakini zaidi tukijali kuukomboa wakati.
Waefeso 5:15 – 16

Kitu kimoja, ambacho pia ni hazina ya msingi sana ni muda, na kwakutokutumia muda vema wengi tunapoteza sana muda tukifanya mambo yasiyo ya msingi.

Tuesday, June 25, 2013

Twonane Milele

1. Nyimbo na tuziimbe tena
    Za alivyotupenda mbele;
    Kwa damu ya thamani sana!
    Mbinguni hwonana milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
2. Hupozwa kila aoshwaye
    Kwa damu ya kondoo yule;
    Ataishi afurahiye
    Vya Yesu Mbinguni milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
3. Hata sasa hufurahia
    Tamu yake mapenzi yale,
    Je, kwake tukifikilia,
    Kutofarakana milele?
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
4. Twende mbele kwa jina lake
    Hata aje Mwokozi yule,
    Atatukaribisha kwake,
    Tutawale naye milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.
 
5. Sauti zetu tuinue
    Kumsifu Mwokozi yule,
    Ili watu wote wajue
    Wokovu u kwake milele.
 
Twonane milele,
Twonane bandarini kule;
Twonane milele,
Twonane bandarini kule.

Monday, June 24, 2013

Kujishusha


Matatizo mengi katika jamii yetu yanatokana na kila mmoja kujiinua, kutaka kutambulika (umaarufu), pia kwasababu hatuna roho ya kujishusha.
Migogoro mingi katika familia ni kwa kuwa kina mama wanataka kuwa nafasi sawa na kina baba, wakijua kwamba wana uwezo wa kumudu majukumu, zaidi mpango wa haki sawa kwa wote umebadilisha kabisa maadili katika jamii nzima.
Mwanzo 3:16
Matatizo mengi katika maeneo ya kazi pia yanatokana na kutojishusha kwa mfanyakazi au mwajiriwa ambaye anaona anajua zaidi kuliko mkubwa wake, ama ni haki yake. Nakumbuka wakati mmoja mama yangu aliniambia kuwa “mwanangu mkubwa hakosei”, na si kwamba mama alimaanisha kuwa hakika mkubwa hakosei ila yampasa mdogo kushuka.
Mwanzo 39:11 – 19
Yusufu alikuwa na kila sababu ya kujitetea na kupignia haki yake, lakini aliamua kujishusha akiamini kwamba ndivyo inavyompasa kuenenda na kufanya, na hakika alimuona Mungu akimpigania na kumuinua hata alipokuwa gerezani.
Bwana wetu Yesu alijishusha sana hata kufikia mauti ya msalaba. Ingawa Yeye ni mfalme wa wafalme, lakini hakuishi katika jumba la kifaari, zaidi alipiga kambi na wanafunzi wake popote. Lakini pia, hata alipokamatwa, akateswa sana na kutemewa mate na kuishia msalabani, alisema “Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo”. Lakini, katika kujishusha kote huku ndipo tumepata wokovu mkuu na ulio wa thamani sana leo hii.
Mathayo 8:20 | Luka 23:34
Yakobo 4:10
Mtu anayejishusha siku zote Mungu humuinua sana. Zaidi, kujishusha ni kutohesabu vingapi tunapoteza ila kuachia kusudi la Mungu liweze kutimia katika maisha yetu. Mwizi anapokuja kuiba hazina yako ambayo Mungu alikusudia iwe yako, ataambulia kuchuma laana, lakini wewe utamuona Mungu akikubariki kwa hazina zaidi.
Warumi 12:20
Unapomsaidia adui kwa moyo mkunjufu, unakuwa umejishusha kwa kiasi kikubwa sana kwakuwa katika uhitaji wake kwa hali ya kawaida ndio wakati mzuri wa kulipa kisasi. Tukikumbuka Daudi alivyojishusha kwa Sauli mara mbili hata asimuue, na Mungu alimbariki na kumuinua Daudi.
Kujishusha kunaghairi mabaya, hata kosa likasamehewa na kusahaulika. Abigaili alivyojishusha na kumuokoa mumewe Nabali asiuliwe na Daudi, hata Daudi akakubali ombi na kughairi uteketezaji aliokuwa amenuia nyumbani kwa Nabal.
1 Samweli 25:23 – 35
Kujishusha ni tabia ya Mungu ndani yetu, hivyo tunapojishusha tunasababisha watu waione nuru ya Mungu ikiwaangazia, ndio maana mtume Paulo alijishusha sana katika huduma yake. Kujishusha hakutizami tunapoteza mangapi katika mwili bali tunaweka hazina kiasi gani Mbinguni kwa Baba yetu.

Hesabu Baraka


Maisha yetu kwa sehemu kubwa sana yamejawa na mtazamo wa kutizama ni kipi ambacho hatuna, ama ni wapi ambapo tunahangaika daima. Hakika duniani tunayo dhiki, lakini katika uhalisia tumebarikiwa sana kuliko dhiki tulizonazo, zaidi sana dhiki yetu ni ya kitambo kifupi tu.
Tunapohesabu baraka, tunaruhusu ukuu na uweza wa Mungu uonekane katika maisha yetu siku zote, zaidi tunaweza kuona na kujua kuwa Mungu yuko kazini akijishughulisha kwa ajili ya mambo yetu kuliko ambavyo tunaweza kutafakari na kuona.
Zaburi 100:4
Ukimtizama mtoto mdogo, anajua kuwa kila kitu kipo, tena anajua kuwa baba ana pesa ya kutosha kumnunulia kila anachohitaji, ndio maana siku zote watoto wana furaha na amani. Lakini pia watoto hawajui kupima uzito wa mahitaji muhimu, hivyo hatutakiwi kuwa kama watoto katika hili bali tutafakari siku zote mema ambayo Mungu ametufanyia na kushukuru tukimsifu daima.
Kubarikiwa si kuwa na majumba ya kifahari, wala magari na pesa nyingi bali kuwa mzima mwenye afya tele pamoja na amani ipitilizayo amani zote tukipata kibali kila tuendapo. Kubarikiwa pia ni kumjua sana Mungu tukizishika amri zake.
Ayubu 22:21
Mtu anapobarikiwa na Mungu, anatosheka anakuwa hana uhitaji tena, ndio maana Bwana Yesu alimwambia yule mwanamke Msamaria kuwa akinywa maji atakayompa Yeye hakika hataona kiu tena. Kitu chochote kile kilichobarikiwa na Mungu kinatosha kabisa wala hakihitaji nyongeza. Lakini tunapokuwa na mali ama utajiri ila tunahitaji kupata zaidi inabidi tujikague na kumuuliza Mungu kuwa ni baraka toka kwake au lah, kwa maana wengi wameacha kumuabudu Mungu wakaabudu mali na utajiri.
Yakobo 3:10
Mungu ametupa uwezo wa kujitamkia na kuwatamkia wengine laana au baraka, lakini mara nyingi tunatumia ndimi wetu kulaani badala ya kubariki. Mara nyingi tunajiambia kwamba hii kazi ikiisha sijui itakuwaje, ama siwezi kufanya biashara, au mke wangu ni mkorofi sana, ama watoto wangu ni wakaidi mno, au sidhani kama nitafanikiwa daima pamoja na mengine mengi. Haya pia huwa tunayazungumza kwa wengine hata tukawalaani.
Warumi 12:2
Kwa Mungu wetu hakuna laana, wala magomvi yoyote bali kuna amani, upendo, upole pamoja na baraka tele. Mataifa huenenda wakitizama nini au kipi wanakosa na wapi wamepungukiwa wakizidi kuona kwamba hakika maisha hayawatendei haki, bali sisi si wa dunia tena na haitupasi kuenenda kama wao.
Wafilipi 4:8
Inatupasa kutambua baraka zetu kama jinsi ambavyo zinatuzunguka, lakini pia inatubidi kukiri baraka hata kabla hatujaziona kwa macho ya nyama, cha msingi tumeshamuomba MUngu na kuamini hakika itakuwa sawa sawa na kuamini kwetu.

Wednesday, June 19, 2013

Liko Lango Moja Wazi

1. Liko lango moja wazi,
    Ni lango la Mbinguni;
    Na wote waingiao
    Watapata nafasi.
 
Lango ndiye Yesu Bwana
Wote waingie kwake,
Lango! Lango
La Mbinguni ni wazi.
 
2. Yesu ndiye lango hili,
    Hata sasa ni wazi,
    Kwa wakubwa na wadogo,
    Tajiri na maskini.
 
Lango ndiye Yesu Bwana
Wote waingie kwake,
Lango! Lango
La Mbinguni ni wazi.
 
3. Hili ni lango la raha,
    Ni lango la rehema;
    Kila mtu apitaye
    Hana majonzi tena.
 
Lango ndiye Yesu Bwana
Wote waingie kwake,
Lango! Lango
La Mbinguni ni wazi.
 
4. Tukipita lango hili
    Tutatua mizigo
    Tuliyochukua kwanza,
    Tutavikwa uzima.
 
Lango ndiye Yesu Bwana
Wote waingie kwake,
Lango! Lango
La Mbinguni ni wazi.
 
5. Hima ndugu tuingie
    Lango halijafungwa,
    Likifungwa mara moja
    Halitafunguliwa.
 
Lango ndiye Yesu Bwana
Wote waingie kwake,
Lango! Lango
La Mbinguni ni wazi.

Tuesday, June 18, 2013

Kazi Yangu Ikiisha

1. Kazi yangu ikiisha, nami nikiokoka;
    Na kuvaa kutokuharibika,
    Nitamjua Mwokozi nifikapo ng'amboni;
    Atakuwa wa kwanza kunilaki.
 
Nitamjua, nitamjua, nikimwona uso kwa uso;
Nitamjua, nitamjua, kwa alama za misumari.
 
2. Furaha nitapata nikiona makao
    Bwana aliyotuandalia;
    Nitamsifu Mwokozi kwa rehema na pendo
    Vilivyonipa pahali mbinguni.
 
Nitamjua, nitamjua, nikimwona uso kwa uso;
Nitamjua, nitamjua, kwa alama za misumari.
 
3. Nao waliokufa katika Bwana Yesu,
    Nitawaona tena huko juu;
    Lakini nifikapo kwake huko Mbinguni,
    Nataka kumwona Mwokozi kwanza.
 
Nitamjua, nitamjua, nikimwona uso kwa uso;
Nitamjua, nitamjua, kwa alama za misumari.
 
4. Milangoni mwa mji Bwana atanipisha,
    Pasipo machozi wala huzuni.
    Nitauimba wimbo wa milele; lakini
    Nataka kumwona Mwokozi kwanza.
 
Nitamjua, nitamjua, nikimwona uso kwa uso;
Nitamjua, nitamjua, kwa alama za misumari.

Friday, June 14, 2013

Ni Salama Rohoni Mwangu

1. Nionapo amani kama shwari,
    Ama nionapo shida;
    Kwa mambo yote umenijulisha
    Ni salama rohoni mwangu.
 
         Salama rohoni,
         Ni salama rohoni mwangu.
 
2. Ingawa Shetani atanitesa,
    Nitajipa moyo kwani
    Kristo ameona unyonge wangu,
    Amekufa kwa roho yangu.
 
         Salama rohoni,
         Ni salama rohoni mwangu.
 
3. Dhambi zangu zote, wala si nusu,
    Zimewekwa Msalabani;
    Wala sichukui laana yake,
    Ni salama rohoni mwangu.
 
         Salama rohoni,
         Ni salama rohoni mwangu.
 
4. Ee Bwana himiza siku ya kuja,
    Panda itakapolia;
    Utakaposhuka sitaogopa -
    Ni salama rohoni mwangu.
 
         Salama rohoni,
         Ni salama rohoni mwangu.

Thursday, June 13, 2013

Furaha Huja Asubuhi


Kuiona siku nyingine mpya ni upendeleo, zaidi ni baraka ya pekee sana kutoka kwa Mungu wetu ingawa kwa wengi wetu hatujui uthamani wa kuiona tena siku nyingine ila inakuwa ni kawaida tu au mazoea yasiyobeba uzito wowote.
Mungu wetu ametujalia furaha ya kuwa nayo siku zote na wakati wote, ingawa muda mwingi na katika mambo mengi tunachagua kuwa na hofu tukihuzunika sana. Jambo moja la msingi kukumbuka siku zote ni kwamba kinachotutenganisha sisi na furaha ni kutokulijua Neno la Mungu, maana Neno linatuambia wazi majonzi hudumu usiku lakini furaha huja asubuhi.
Zaburi 30:5

KInachotuumiza ni kwakuwa tunaamua kuhangaikia sana vile ambayo havitakiwi kuhangaikiwa, pia hatujui namna ya kuthamanisha vile tulivyonavyo tukishukuru na kumtukuza Mungu, ndio maana siku zote tunajiona sisi ni wahitaji tu, zaidi haijawahi kufikia siku tukatosheka.
Mathayo 6:25 – 34 | 1 Timotheo 6:6 – 10
Wengi tunajawa na hasira pamoja na uchungu kutokana na matukio mbali mbali yanayotukuta kwenye maisha yetu ya kila siku, pia hatuwezi kuizuia hasira kutufika wala uchungu lakini hatutakiwi kuviruhusu vitutawale maishani mwetu. Hata kwenye msiba wanaomboleza kwa muda, lakini wakiendelea kuomboleza siku zote ina maana wameamua kubadili mfumo wa maisha Mungu aliouweka kabisa. Tunapoishi kwa maumivu ya jana au siku za nyuma ina maana tumeamua kuikataa leo.
Zaburi 118:24
Mtumishi wa Mungu Daudi alilitambua kwamba kila siku ni mpya, na inampasa kushangilia na kushukuru katika hiyo. Nasi inatupasa kubadili namna ya maisha yetu, tukubali kwa yote yaliyopita hakika hatuwezi kuyabadilisha ila tunaweza kuanza sasa na kufanya yaliyo mema zaidi mbele za Mungu na jirani zetu.
Tunapoikataa furaha asubuhi tunampa shetani nafasi kuiteka siku yetu, ndio maana kuna watu wanasema wameamka vibaya ingawa hawaumwi ila anakuwa na hasira tu siku nzima wala hajisikii kufanya kitu chochote. Cha msingi cha kufahamu ni kwamba furaha ni chaguo kama ambavyo huzuni pia ni chaguo la mtu binafsi. Ndio maana Joshua aliwaambia wana wa Israeli wachague ni nani watakayemtumikia ila yeye na nyumba yake wanamtumikia Bwana.
Joshua 24:15
Tunapoamka asubuhi tunatizama nini? Tunakumbuka jana ilikuwa mbaya kiasi gani, tunatizama ni vingapi ambavyo tunahitaji lakini hatuna au tunatizama jinsi ambavyo hatuko kama wengine? Haya yote tunapoyatizama yanatuletea huzuni siku nzima, lakini tukiangalia uhalisia wa kwamba ni siku nyingine mpya, tukamshukuru Mungu kwa uzima na afya njema, tukaona taswira ya Mungu ndani yetu, na kujua kuwa Mungu yupo kazini kutubariki, kututetea, kutupigania na kutuongoza; hakika hatutakuwa na muda wa kuikumbatia huzuni na hasira.
Furaha ni hali inayokosekana kwa watu wengi sana, hata tunakosa amani moyoni pengine hata kukata tamaa ya maisha kabisa. Siri moja ya msingi, inatakiwa tufurahie kwanza vile tulivyonavyo, zaidi sana jinsi tulivyo ndipo tutasababisha Mungu atubariki kwa vingine vingi zaidi.

Twende Kwa Yesu

1. Twende kwa Yesu mimi nawe,
    Njia atwonya tuijue
    Imo Chuoni; na Mwenyewe,
    Hapa asema, Njoo!
 
         Na furaha tutaiona,
         Mioyo ikitakata sana,
         Kwako, Mwokozi, kuonana,
         Na milele kukaa.
 
2. "Wana na waje" atwambia,
    Furahini mkisikia,
    Ndiye mfalme wetu pia,
    Na tumtii, Njoo.
 
        Na furaha tutaiona,
        Mioyo ikitakata sana,
        Kwako, Mwokozi, kuonana,
        Na milele kukaa.
 
3. Wangojeani? Leo yupo;
    Sikiza sana asemapo;
    Huruma zake zikwitapo,
    Ewe kijana, Njoo.
 
       Na furaha tutaiona,
       Mioyo ikitakata sana,
       Kwako, Mwokozi, kuonana,
       Na milele kukaa.

Wednesday, June 12, 2013

Twasoma Ni Njema Sana

1. Twasoma, ni njema sana
    Mbinguni, kwa Bwana;
    Twasoma, dhambi hapana,
    Mbinguni, kwa Bwana;
    Malaika wema wako,
    Vinanda vizuri viko,
    Na majumba tele yako,
    Mbinguni kwa Bwana.

2. Siku zote ni mchana,
    Ni nchi ya raha;
    Wala machozi hapana,
    Ni nchi ya raha;
    Walioko wauona
    Uso wa Mwokozi, tena
    Jua jingine hapana,
    Ni nchi ya raha.

3. Nyama na vitu viovu
    Havimo kabisa;
    Kifo nacho, na ubovu,
    Havimo kabisa,
    Ni watakatifu wote,
    Wameoshwa dhambi zote;
    Wasiosafiwa wote
    Hawamo kabisa.

4. Tuna dhambi pia sote,
    Mwokozi akafa;
    Kwake tutaoshwa zote,
    Mwokozi akafa;
    Kwake twapata wokovu,
    Tutawona utukufu;
    Mbinguni tutamsifu;
    Mwokozi akafa.

5. Baba, mama, ndugu zetu,
    Twendeni kwa Bwana;
    Huku chini siko kwetu,
    Twendeni kwa Bwana;
    Tusishikwe na dunia,
    Na dhambi kutulemea,
    Tutupe vya chini pia,
    Twendeni kwa Bwana.

Tuesday, June 11, 2013

Roho Ya Heshima

Heshima ni kitu cha msingi sana katika maisha ya jamii, kiasi kwamba mahali penye heshima panatawaliwa na upendo pamoja na Amani.
Jamii tunayoishi imetawaliwa na dharau inayojengeka kutokana na mali, nafasi katika nyadhifa fulani pia elimu ambapo ni tofauti kabisa na mpango wa Mungu, kwani inatupasa kumheshimu kila mmoja haijalishi ni mkubwa au mdogo zaidi anacho au hana.
1 Timotheo 5:1 – 2
Mara nyingi tunakosa kubarikiwa kwa sababu ya jambo ambalo tunasema au kushabikia tukimkosea heshima ndugu, jamaa, mzazi na hata mtumishi wa Mungu kwakuwa tunaona yamkini kile alichokifanya si sahihi, ila jambo la msingi kukumbuka siku zote ni kwamba ile nafasi aliyonayo mhusika sisi hatujamuweka ila Mungu, na katika kumkosea heshima kwetu kitakachotupata ni laana.
Hesabu 12:1 – 14
Mambo mengi sana tunafanya au kusema tukiwakosea heshima wengine kwa kuiga au kufuata mkumbo wa wengine au jamii inasemaje, lakini tukumbuke kuwa katika mengi sana jamii huwa inakosea hivyo Neno la Mungu inabidi likae kwa wingi ndani yetu na kutuongoza siku zote.
Kutoka 20:12
Haijalishi mzazi ana kasoro ya namna gani, au anafanya makosa kiasi gani yamkini amekuwa mbaya kwako kwa mangapi lakini siku zote tunatakiwa kumheshimu na kumshukuru Mungu kwa yote. Kuwa na mzazi bado ni bahati sana maana wapo ambao hawana hata mmoja, zaidi tusipoweza kumheshimu mzazi tunayemuona haiwezekani kumheshimu Mungu tusiyemuona.
Mara nyingi sana tumesikia na kushuhudia yamkini nasi tumeshiriki kwa sehemu kuwasema vibaya viongozi wa ngazi fulani katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini. Ikiwa kuna baya lolote au popote pale ambapo wamekosema, sio jukumu letu sisi kuwahukumu na kuwakosoa kwa namna ya kuwakosea heshima lah, ila siku zote hukumu ni juu ya Mungu kuwarekebisha yeye, sisi yatupata kuheshimu tukiitii mamlaka.
Daniel 3:8 – 30
Ingawa Shedrack, Meshack and Abed-Nego walimwabudu Mungu wa kweli, pia ilikuwa haki kwako  kutokuanguka na kuisujudia sanamu ya mfalme Nebuchadnezzer, hata hivyo walitunza heshima yao juu ya mfalme kwa jinsi walivyomjibu kabla pia baada ya kuingizwa kwenye tanuru la moto lilikokuwa limechochewa mara saba zaidi.
Tumuombe sana Mungu wetu atujengee roho ya heshima ndani yetu, zaidi heshima ni kitu cha bure ambacho hakikugharimu unapokitoa zaidi unapata akiba ya Baraka ambapo kwa wakati Mungu anakuinua. Wenye roho ya heshima wanafika mbali sana katika maisha wakimuona Mungu akitenda mambo makuu na kuwapigania sana.

Mbegu Inakufa Ili Izae


Matunda mengi sana yanayoliwa hata yale yasiyoliwa yana mbegu moja au Zaidi ndani yake, na mbegu hizo zinaendeleza kizazi cha hilo tunda au muendelezo wa kuwepo kwa tunda kwa kadri maisha yanavyoendelea.
Mafanikio ya mbegu yoyote ni kuchipua ardhini hata ikawa mmea au mti uliokomaa na kuzaa matunda mazuri yatakayoiva, lakini mbegu isipofanikiwa kuchipua mti imeshindwa katika yote hivyo pia ilikuwa haifai maana kusudi lake hasa halijatimia.
Katika safari yetu ya kuelekea mbinguni haiwezekani kutenda mema na kumpendeza Mungu, zaidi sana kuwa watakatifu kama Yeye alivyo mtakatifu kama hatutakufa kwanza halafu tukafufuka, yaani ule utu wetu wa kale ambao unaambatana na tabia zote za asili hautazikwa ili tufufuke tukiwa viumbe wapya.
Yohana 3:3 – 7
Siku zote za maisha yetu inatupasa kujichunguza sana ili tujue pia kukubari mapungufu ndani yetu, yamkini tabia za asili bado zinatutawala. Mbegu inapofukiwa ardhini huwa inakufa kwanza hata iweze kuchipua upya. Unapoitizama mbegu iliyokufa (sio kuoza), lile ganda lake linakuwa limechoka na kuchakaa hata kushindwa kuzuia kile cha ndani yake kuchukua nafasi kutoka nje.
Miili yetu inapoachwa ikachakaa na kuchoka kabisa (kutokuhisi chochote kile cha dunia hii katika mwili wa nyama) ndipo pale tunapompa nafasi Roho wa Mungu akatawale na kutuongoza katika mema yote.
2 Wakorintho 5:17
Ipo mimea ambayo inadumaa, ama imechipua vema ila haizai matunda siku zote kiasi kwamba hatuipendi kwakuwa haina faida yoyote kwetu zaidi ya kuwa mmea au mti tu lakini kusudi lake hasa halijatimia, ndio maana tunapojichunguza inawezekana kabisa tumechipua lakini hatukui, au tunakua lakini hatuzai matunda wala hakuna dalili ya kuzaa matunda kwa sababu utu wetu wa kale bado umo ndani yetu, ama yamkini bado tunaipenda dunia kwa kiasi Fulani, na hatujataka kuiacha miili yetu ya nyama kufa kabisa.
Yohana 15:1 – 8
Siku zote mbegu inayopandwa katika udongo mzuri huzaa sana, vivyo hivyo nasi inatupasa tujiweke kwenye mazingira mazuri ya kukua kiroho, kuondokana na vishawishi vya tamaa na tabia za dunia hii kuchukua nafasi tena katika maisha yetu hata tukarudi nyuma kabisa ama kuwa vuguvugu.
Tunapokuwa kwenye mazingira sahihi ya kiroho na kimwili hakika tunauona utukufu wa Mungu ukituzunguka muda wote na kutawala maisha yetu, maana Mungu huwa hatuachi bali dhambi zetu wenyewe zinatutenganisha na uwepo wa Mungu, kama ambavyo mbegu iko tayari kufa ili ichipue tena na kuzaa lakini kuiteketeza mbegu ni kuiweka katika mazingira yasiyofaa.
Isaya 59:2

Kushindwa Unapokuwa Ni Ushindi


Katika maisha ya mwanadamu yoyote, maamuzi ni jambo la msingi sana tena la kuzingatia muda wote. Lakini maamuzi yanapofanyika kwa hekima na busara ya Mungu ili yawe sahihi, siku zote yanaleta matokeo ambayo ni sahihi na mazuri, maana sote tunaishi leo kutokana na maamuzi ambayo tuliyafanya jana, pia kesho kwa maamuzi tunayoyafanya leo.

Mtoto mdogo anapochukua uamuzi wa kujifunza kutembea, anaanza na hatua moja, ambayo itapelekea kupiga hatua ya pili hata ya tatu kabla hajadondoka. Ingawa kudondoka kunaonyesha hajatimiza lengo lakini bado hajashindwa ingawa kwa mwenzake anayetembea ataonekana kashindwa.

Daudi alipukuwa akikimbia ili kuokoa maisha yake toka mikononi mwa Sauli hakika alionekana ameshindwa kumkabili Sauli, hata ile hali ya ushujaa haikuonekana kwake. Zaidi hata mahali ambapo Daudi alipata fulsa mara mbili ya kuweza kumuua Sauli bila kufanya hivyo, hata wenzake naamini walimuona amekuwa dhaifu.
1 Samueli 24:5 – 7 | 1 Samueli 26:9 – 10

Kinachotuponza wengi ni kujihimu ili tuonekane kama wengine wanaotuzunguka, ili tupate umaarufu kuwa hakika tumeweza kukabiliana na mtu au jambo bila kujua kwamba tunajijengea utukufu na kujiinua ambapo si muda vitatuangamiza sisi wenyewe.
Yakobo 4:10 | Mithali 16:18

Daudi aliamua kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika mpango wa Mungu, na hakika katika wakati uliostahiki akawa mfalme, maana hatimaye Mungu aliamua kati yake na Sauli.
Wafilisti walipofanikiwa kumkamata Samsoni, wakamng’oa macho waliamini kwamba hakika huo ndio mwisho wa nguvu zake, na kati ya mambo waliyofanikiwa kushinda hilo lilikuwa mojawapo maana Samsoni aliwasumbua sana.

Naamini Samsoni alifahamu jambo moja kwamba kushindwa kwake ni ushindi kwani kusudi la Mungu hakika lazima litimie, hata alipokuwa akisaga ngano nywele zake zikaanza kuota tena, akajua hakika kinachompasa ni kupiga hatua na kufanya maamuzi sahihi katika mpango wa Mungu, na hakika Samsoni akaua watu wengi zaidi wakati wa kifo chake kuliko hapo awali.
Waamuzi 16:23 – 30

Mungu ametukabidhi zana zote kuhakikisha kwamba tunashinda na kusudi lake linatimia, haijalishi tunatereza au kuanguka mara ngapi ila cha msingi ni maamuzi tuliyoamua na kunuia kuyafanya katika kusudi la Mungu ni lazima yatimie.

Inawezekana kabisa kuna nyakati tunakata tamaa, inawezekana nyakati fulani tunashindwa kuvumilia, lakini tumkumbuke Yusufu ambaye alivumilia na kusamehe yote ingawa ndugu zake waliona wameshammaliza hata ndoto zake hazitatimia.

Tumtizame pia Bwana wetu Yesu ambaye alinyenyekea hata mauti ya msalaba, hata akaonekana ameshindwa kabisa maana hakujinasua toka msalabani, lakini siku ya tatu alifufuka akiwa mshindi wa yote.