Mathayo 24:12
Kwa kizazi cha zama hizi maasi yamekuwa ni jambo la kawaida
sana, zaidi yamekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kila tunapokwenda
na tunapokuwa maasi yanatuzunguka kiasi cha kuwanasa hata wanaoenenda katika
njia ya haki.
Kuongezeka kwa maasi kunakwenda sambamba na upendo kupoa, na
upendo unapopoa ndani yetu ina maana nafasi ya Mungu kwetu inakuwa haipo
kwasababu Mungu ni pendo (1 Yohana 4:8),
na kwa jinsi hii Shetani atatawala, kwakuwa nuru tena haipo.
Maasi huenea pale mwanadamu anapomsahau Mungu, akaanza ibada
ya sanamu kwa kuvipa vitu vingine umuhimu na kipaumbele kuliko Mungu, ndipo
anakuwa katika nafasi ya kufanya chochote kile ili kutimiza azma yake
pasipokuwa na hofu yoyote juu ya Mungu wake aliyemuumba, yaani anakuwa amekufa
kabisa kiroho ingawa katika mwili bado anaishi, na ikiendelea hivyo inafikia
hatua ya kuamini kuwa hakuna Mungu kwasababu anaona yote anayafanikisha kwa
uwezo na jitihada zake.
Inatisha sana pale maasi yanapotuteka watenda haki wa Mungu,
na si kwamba yanatuteka kwakuwa yamekuwa na nguvu sana, hasha! (1 Yohana 4:4) Kwahiyo tunapofikia hatua
ya kutekwa na uovu ina maana tumeamua kuchukuliana nao hata tukafikia hatua ya
kutamani tukiona kuwa yamekuwa njia sahihi ya kuiendea.
Chanzo kikubwa sana cha maasi ni kupolomoka kwa maadili
katika jamii, kiasi kwamba mambo ambayo yalikuwa ni aibu kuonekana yakifanyika
sasa yanakubalika na kuwa jambo au tukio la kawaida kabisa. Badala ya kuzishika
amri za Mungu, watu wanajisifia kwa kuzikiuka, na inaonekana kuwa ni jambo la
kawaida kabisa. Mbaya zaidi wazazi wamekuwa mfano mbaya sana kwa watoto wao,
ndio maana watoto wanajifunza kile wanachokiona kwa wazazi wao, na si
vinginevyo.
Tunaweza kuepukana na maasi endapo tutaamua kubadilika
tukimtafuta Mungu kwa bidii zote ili atuonyeshe namna ya kuenenda (Zaburi 32:8). Lakini pia inatupasa
kujiweka mbali na kupenda pesa, maana ndiyo mwanzo wa maovu yote (1 Timotheo 6:10 | Mathayo 6:24).