Pages

Nataka Kuokoka Sasa Hivi!

Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.

Tuesday, February 14, 2012

Uvumilivu Ndani ya Yesu


Mathayo 24:13 yeye atakayevumia hata mwisho, huyo ataokoka.

Maisha ya wokovu ni tamaduni pia desturi ya kujikana sana; na kutokana na kujikana huko unakuja uvumilivu. Mathayo 16:24

Kutokana na uhalisia huo ndio maana safari ya wokovu inakuwa ngumu sana hasa tunapokuwa katika hali ya mwili huu, kwakuwa mwili una kila hisia na mahitaji. Tunapotizama wenzetu wakifanikiwa na kuishi kwa furaha kutokana na njia zao potofu nasi tunajitahidi bila mafanikio inakatisha sana tamaa; lakini inahitaji sana imani na uvumilivu wa ziada kuweza kusonga mbele.
Yakobo 4:4 …rafiki wa ulimwengu ni adui wa Mungu.

Wengi wetu mara tu baada ya kuokoka tulikutana na majaribu tofauti kama kukataliwa na wazazi, marafiki kututenga, kutokubalika tena kazini hata jamii nzima. Kipimo cha imani ni pale unapokuwa huna kitu, huna msaada wala huna yeyote ila Yesu tu. Yohana 16:33

Mitume wasingekuwa na uvumilivu sisi leo hii tusingekuwa tunasoma habari njema za ufalme wa Mungu, lakini kutokana na uvumilivu wao ulio mkuu hata leo tunayo neema ya biblia; lakini zaidi ya yote endapo Bwana Yesu asingevumilia mateso hata kufia msalabani leo sisi tungekuwa wapi?

Siku zote inabidi tumuombe Mungu sana kuweza kushinda vishawishi pia majaribu ya adui zetu watatu; ambao ni MWILI | ULIMWENGU | SHETANI. Bila kuweza kuvumilia na kushinda tamaa za mwili, ulimwengu na majaribu ya Shetani hakika tutaishia kwenye moto wa milele.

Mhubiri Billy Graham alisema endapo kuna watu ambao leo Mungu anaweza kuwarudisha wakaishi akiamini watashinda yote ni Ayubu ambaye alimshinda Shetani, Nuhu aliyeushinda ulimwengu na Daniel aliyeushinda mwili.

Inakuwaje unamkana Yesu kwa mlo mmoja, pengine kwa kazi ya kitambo kifupi, au kwa nyumba nzuri yenye thamani nzuri za kupendeza, au kwa ajili ya mwanamke au mwanaume unayempenda sana; yamkini kwa ajili ya mtoto wako au mwili wako? Mathayo 10:37 – 38 | Mhubiri 3:20 | 1 Timotheo 6:10

Katika yote ni ubatili mtupu hapa duniani, hivyo inatupasa kuvumilia daima na kusonga mbele bila kukata tamaa.

Baba mmoja na mtoto wake (John) walikwenda safari ya mbali kwa gari, hata walipokuwa wakisafiri wakienda na kuuacha mji kabisa wakaingia kwenye nyika na kuzimaliza hata kufika kwenye jangwa ambapo kwa Bahati mbaya gari lao likatitia kwenye mchanga. Jitihada za kuitoa hazikuzaa matunda kwani kadri walivyojaribu ndivyo ikazidi kutitia. Baba akamwambia mwanaye kuwa inabidi atembee kurudi mjini kutafuta msaada ambapo itamchukua siku moja au zaidi hivyo yeye inabidi abaki kumsubiri pale. John akamtizama baba yake akienda na kutokomea kabisa hata giza likaingia, lakini kila alipokuwa akiwaza alikumbuka kuwa baba amesema anakwenda kutafuta msaada na atarudi kunichukua.

Basi wapendwa tusikate tamaa, tuwe na uvumilivu maana Yeye ajaye hatakawia maana kwa wakati wake atakuja kutuchukua.  Yohana 14:1 – 4

No comments:

Post a Comment