Tunakata tamaa siku zote baada ya
kuona yote tuliyojaribu yameshindikana, pia hakuna anayewezakutusaidia ama
uwezo wa kila mmoja kando yetu umefikia kikomo; hapo sasa tunakubali matokeo
kwamba tumefika mwisho na tumeshindwa.
Haiba moja kwetu siku zote ni
kuyatizama mambo katika ugumu wake wala si katika urahisi wake, hivyo kinachotujia
akilini ni kwamba haiwezekani wala haitawezekana.
Mwanzo 37 – 41, Yusufu ni kati ya watu waliokatishwa tamaa sana
ikiwa ni pamoja na ndugu zake; baba yake alimkemea kuhusu ndoto zake, ndugu
zake wakamuuza, Potifa akamuweka gerezani, Mnyweshaji alimsahau alipotolewa
gerezani lakini kutokukata kwake tamaa kulimuinua juu ya wote. Kumbuka unaweza
kumuangamiza muota ndoto lakini sio ndoto ya Mungu.
1 Samweli 17: 33, Daudi hakuhofia uzoefu wala ukubwa wa Goliati
kwenye vita lakini alimuamini Mungu muweza yote. Daudi pia aliishi kwa muda
mrefu mafichoni akikimbia kuuawa na Sauli, lakini hakukata tamaa kwamba ufalme
alioahidiwa sio wake tena, ila aliamini kwa wakati Mungu atamuweka
anapostahili. 1 Samweli 19: -
Samsoni alilaghaiwa na Delila,
akakamatwa na kupofuliwa macho kisha akawekwa gerezani akisaga ngano. Lakini
mwishoni walipomtoa kwenye ukumbi wa maonyesho ili awafanyie michezo, pale
akasimama akishikilia nguzo mbili kuu za ukumbi, akamuomba Mungu amrejeshee
nguvu zake walau mara moja alipe kisasi, maana aliamini inawezekana kwakuwa
hakukata tamaa. Waamuzi 16:26 - 30
Mara nyingi tunakuwa kwenye
mazingira magumu sana, masomoni, kazini hata nyumbani tukiona mambo hayaendi,
kila tunachojaribu hakifanikiwi wala hakuna anayetuunga mkono, ila leo Mungu
ana jambo nawe kuwa usikate tamaa kamwe maana ahadi zake ni za kweli tena za
milele.
Inawezekana una kilema; umeokoka
ila bado tamaa imekushika, bado unasema uongo, hujaacha udokozi, usengenyaji,
pengine unaonjaonja pombe au sigara na pengine umejihalalishia mke wa pembeni
ingawa siku zote inakuuma sana, na unataka kuacha ila shetani bado kakukamata
kwenye kilema chako. Cha msingi ndugu yangu usikate tamaa, endelea kuomba kwa
bidii na kufunga wala usimsikilize shetani akuhubirie maana yeye ni baba wa
uongo, na zaidi ya yote ni mshitaki wetu daima.
Mark 10:27, Kwa Mungu yote yanawezekana, Pia kila jambo
linawezekana kwake yeye aaminiye.
Ukitereza usikubali kubaki chini,
na ukianguka inuka haraka usonge mbele wala usiangalie watu wanasemaje juu yako
au wanakutizama vipi bali wewe mtizame Mungu ndiye anayetuwezesha katika yote.
Naamini Mungu anapendezwa na watu
wasiokata tamaa, maana anapoona shetani akikujaribu hata zaidi ya mara elfu
moja nawe unasimama tu na kusonga mbele ama kwa hakika ataingilia kati, lakini
ukishasema siwezi tena unakuwa umempa shetani ushindi usio wa lazima. Inawezekana
pia kwa kuangalia umbali tukiotoka tunakata tama kabisa, lakini kwakuwa Bwana
Yesu alishinda, nasi tutashinda na zaidi ya kushinda. Yohana 16:33
No comments:
Post a Comment