Ilimpasa Bwana wetu Yesu Kristo kupitia mateso yote hata kufa ili sisi
tupate kupona pamoja na ukombozi mbali na dhambi, lakini si hilo tu ila tupate
ushindi katika Yeye kwa kukishinda kifo alipofufuka siku ya tatu. Tufurahi
kwani yeye ameshinda yote, hivyo nasi tunapokuwa ndani yake hakika tutashida.
Yohana 16:33
Leo tunakumbuka kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kiristo, lakini
haitakuwa na maana sana kama huyu Yesu hafufuki pamoja nasi miyoyoni mwetu,
haina faida kabisa. Mmoja wa wahalifu kati ya wale wawili aliosurubiwa naye
pale msalabani alimtizama na kusema Bwana unikumbuke utakapoingia katika ufalme
wako.
Luka 23: 42 – 43
Imani ndani ya huyu mhalifu ilikuwa timilifu sana, maana walikuwa na
Yesu msalabani, lakini bado aliamini kwamba hakika huyu ni Mungu mwenye uweza
wote. Lakini katika upande mwingine tunaona jinsi Petro alivyomkana Yesu mara
tatu kwa kukosa Imani, pia baada ya Yesu kufa wanafunzi wake walijifungia kwa
hofu wakijua yote yameishia hapo.
Luka 24: 36 – 42
Inawezekana kabisa kwamba kama
dada zake Lazaro ambao waliamini Yesu anaponya lakini walimuwekea mipaka katika
kufufua, nasi pia inawezekana kabisa kwamba tunamfahamu Yesu na matendo yake
ila Imani timilifu tunakosa, yamkini hata Imani kiasi cha chembe ya haradali tu
ni shida. John 11: 17 – 25, 38 – 44.
Imani timilifu haiji hivi hivi ila ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,
kwani yote yaliyo ya Imani ni yale ya rohoni ambayo hukua hata yakaonekana nje.
Tunaona wanafunzi baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu walitoka kwa ujasiri kwenda
kuihubiri injili.
Matendo ya Mitume 2:14 – 17
Tunapokumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo, inatupasa tukumbuke pia
kupokea ile ahadi aliyotuahidi ya Msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu, ambaye kwa
huyo tutaweza kuitenda kazi katika shamba la Bwana, vinginevyo siku zote hatutaweza
kwa kukosa Imani iliyo timilifu.
Waebrania 11:6
Imani timilifu ni kama ya Stefano
aliyetolewa nje na kupigwa mawe bila kubadili msimamo, pia ni kama ya Paul na
Sila waliofungwa gerezani bila kubadili msimamo, na Imani ya namna hii inapopita
kwenye majaribu inakuwa na nguvu zaidi. Imani timilifu ni kuamini hata kama
hatuoni muujiza, hata kama ni wagonjwa mahututi na zaidi sana hata kama
tumepoteza kila kitu.
Dada mmoja mateka nyakati za vita vya dunia aliandika kwa
kukwangua ukutani kabla hajafa “Naamini katika mwanga hata kama siuoni, naamini
katika upendo hata kama siuhisi na ninaamini katika Mungu hata kama akikaa
kimya”
2 Timotheo 2:13
No comments:
Post a Comment