Ndoto ni kitu kizuri sana, hasa ndoto zenye kujenga na
kutupa motisha. Wengi katika tulipokuwa wadogo tuliota maisha ya namna Fulani,
ambayo ni mazuri sana yenye mafanikio bila kuwa na shida yoyote, lakini kuna
usemi unasema ndoto huwa zinatimia walakini pia huwa hazitimii vile vile.
Kwanini huwa tunanuia au kupanga yaliyo makuu sana lakini
inafikia wakati tunakata tamaa, hata kuona haiwezekani na kurudi nyuma?
Tulipoupokea wokuvu tulikuwa na wito na moto wa hali ya juu sana katika kuitenda
kazi ya Mungu, kusoma na kujifunza neno. Wengine tulinuia kuwa kama watumishi
mbalimbali wakubwa duniani, lakini ile ari sasa imepotea, ule moto umefifia
kama sio kuzima. Je, yale makuu tuliyonuia yameishia wapi?
Kunuia makuu
ni jambo moja, na kufanikisha kile unachonuia ni chambo jingine tofauti kabisa
kwani katika kufanikisha yale makuu tunayonuia siku zote lazima tulifuate na
kulishika neno la Mungu linavyotuambia, vinginevyo hata tukitimiza nia zetu
hazitakuwa za kudumu kwani hazina msingi wa kudumu.
Kuwatumikia wengine
kunamuinua sana mtu siku zote, kama ambavyo Elisha alimtumikia Elia, hata
akamwambia Elia kuwa si kwamba anataka tu kile alicho nacho ila anataka mara
mbili zaidi ya roho iliyokuwa ndani ya yake. 2 Wafalme 2:9 – 14
Wenye uvumilivu siku
zote katika Mungu hufika mbali sana hata kuona yale waliyonuia (ndoto zao)
yakitimia kwa wakati ambao ni timilifu kwa Bwana Yesu, kama ambavyo Neno
linasema kila kilicho kamili hutoka kwa Baba yetu wa Mianga. Yakobo 1:17
Tukimtizama Yusufu ambaye alikuwa akiota, lakini sio kwamba
aliota tu ila aliamini na kuzishikilia ndoto zake hata zitimie, yamkini
angekata tamaa mapema yote yasingewezekana kutimia, hata tunapotizama Yusufu
aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Misri akiwa na miaka 30. Mwanzo 41: 39 – 46
Kung’ang’ania kulimfanya
Jakobo akashindana na malaika, hata akabarikiwa, lakini pia mara zote Eliyah
alipomuambia Elisha asimfuate maana Mungu amemtuma sehemu nyingine, Elisha
alikamjibu kama Mungu aishivyo na roho yako iishivyo sitakuacha kamwe. 2 Wafalme 2: 1 – 2
Usipokata tamaa
unajiweka kwenye nafasi ya kumshawishi Mungu afanye kitu siku zote, maana Daudi
katika magumu yote aliyopitia hakukata tamaa, ingawa aliwindwa sana na Sauli
ili amuue lakini katika yote Daudi alimkabidhi Mungu. 1 Samweli 26:17 – 24
Mapenzi ya Mungu yatimie siku zote katika maisha yetu. Maana, kama tunampenda Yesu, tutampenda na Baba pia, hivyo hatutaishi tukitenda mapenzi yetu ila daima mapenzi ya Baba yatimizwe maishani mwetu. Tukijaribu kulazimisha mambo kwa namna yetu ya akili na maarifa hakika tutakuwa tunapingana na makusudi ya Mungu katika maisha yetu. Mungu anahitaji tumuombe, tujifunze neno lake siku zote na tujinyenyekeze kwake. Yakobo 4:10