Katika maisha ya mwanadamu awaye yoyote, lazima anakuwa na
mahitaji tofauti tofauti kutokana na umri, tamaduni, mila pamoja na mazingira
yanayomkabiri, lakini sote tunajua kuwa mwanadamu asilia ana mahitaji matatu muhimu
ambayo ni chakula, nguo na malazi.
1 Timotheo 6:8
Ukitafakari kwa kina sana, wengi hatuangaiki ili kupata haya
mahitaji matatu ya muhimu sana kwa kila mmoja wetu maana Mungu ndiye
anayehakikisha kuwa katika hivi hatukosi chochote wala kupungukiwa. Ila siku
zote tunahangaika sana kwa vitu vya kupita ambavyo siku zote kadri tunavyopata
huwa hatutosheki hata siku moja.
Usasa na uvumbuzi wa mambo mengi tofauti unatuharibu sana
wanadamu kwa sehemu kubwa badala ya kutusaidia, maana kila siku kuna aina mpya
au kitu kipya ambacho siku zote unapotekwa hakika wewe unakuwa ukihaha bila
kutosheka na kile ulichonacho, siku zote utahitaji zaidi.
Kuna mitindo
ya nguo au viatu; inapotoka tu kila mtu anataka awe nayo ili aonekane anakwenda
na wakati, hata kama atajaza kabati huyu mtu bado hatakuwa katosheka na vile
alivyonavyo. Tizama hata simu, magari na vitu vingine hasa vinavyoonekana mbele
za watu huwa havitupi kutosheka na kukubali kwa kile tulichonacho, lakini zaidi
pia vijana wamekuwa wakibadilisha wenza wao kana kwamba ni bidhaa ya kununua
dukani na kubadilisha kirahisi namna hivyo, yote ni kwa sababu hatutosheki na
kile au yule tuliyenaye.
Mhubiri 1:7 – 8
Unapokula chakula au kunywa maji, unashiba au ile kiu
inaisha kwa wakati huo lakini baada ya muda njaa au kiu itarejea tena. Tofauti
sana kwa upande mwingine ambapo macho huwa hayachoki kuona hata siku moja, pua
nazo hazichoki kunusa wala masikio hayachoki daima kusikia.
Ndio maana mlevi atalewa lakini atataka kuendelea kunywa tu,
na mwizi hawezi kufikia wakati akasema sasa nimeshaiba inatosha, hapana. Mzinzi
au mwasherati siku zote anapatwa na uhitaji wa kuendelea na matendo yake
machafu kwakuwa hawezi kujizuia zaidi sana msukumo unakuwa ndani yake siku
zote. Mtu mwenye mali nyingi siku zote hazimtoshi zaidi anaishi kwa hofu ya
kupoteza zote hivyo daima anataka awenazo nyingi zaidi. Kwa yote ya mwili
hakuna anayetosheka hata siku moja.
Yohana 4:5 – 18
Tumepata Tumaini la milele, Tumaini la kweli ambalo ni
ushindi na habari njema kwa wote wanaosumbuka wakielemewa na njaa pamoja na kiu
zisizokwisha maana Bwana wetu Yesu Kristo ana maji ya uzima, ambayo anatupatia
bure, ila anachotaka kutoka kwetu ni kumuomba Yeye maji haya ya uzima ili
tusisikie kiu wala njaa tena.
Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa! Lakini kizazi hiki kina njaa na kiu ya mitandao ya jamii, simu za mkononi, maisha ya anasa, ulevi pamoja na uzinzi na uasherati. Tumuombe sana Baba yetu wa mbinguni leo aondoe kiu nyingine zote kwetu na jamii nzima, na kujenga ndani yetu njaa na kiu ya haki.
Yesu ndiye maji ya uzima
ReplyDelete