Katika maisha yetu ya kila siku, tunakosea au kukosewa na wenzetu mara nyingi sana, ila zaidi ya yote tunamkosea pia Mungu wetu wa Mbinguni. Ni rahisi sana kuomba msamaha hasa pale tunapokosea wengine, tukitaka tusamehewe kabisa ila kwanini huwa inakuwa ngumu sana kwetu kusamehe na kusahau? Kama umesamehe lakini ujasahau je, huo ni msamaha halisia?
Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasamehe saba mara sabini, kwahiyo haijalishi ndugu yako kakukosea mara ngapi katika jambo moja au mambo tofauti ila inabidi kusamehe mara zote bila kuhesabu gharama na hiki ndicho kitu cha msingi sana maana tusipoweza kusamehe wenzetu tunaowaona hata Baba Yetu wa Mbinguni hataweza kutusamehe sisi makosa yetu.
Mara nyingi tukikosewa, hasira na kinyongo vinajengeka ndani ya mioyo yetu, na hii ni hatari sana kwasababu hatumpi utukufu Mungu hivyo hata roho wake hawezi kukaa sehemu yenye hasira, kinyongo, chuki wala husuda, Mungu wetu atusaidie sana.
Neno la Mungu linasema hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu, ila zaidi ya yote hatutakiwi kukaa na hasira mpaka jua linapozama, na siku zote tukumbuke kuwa leo ni siku njema ambayo Mungu ameiumba hivyo tufurahi na kushukuru katika hiyo maana mbali na magumu yote tunayoyapitia tufahamu kuna wengi ambao walitamani kuwepo lakini hatuko nao tena. Kila leo ni zawadi toka kwa Bwana wa Majeshi.
Neno la Mungu linasisitiza pia kwamba ikitokea ukakwazika na kupatwa na hasira, daima usitende dhambi kutokana na hasira yako maana madhara yake ni makubwa sana. Inawezekana umehuzunika kiasi cha kukosa imani tena, una hasira kiasi cha kuishiwa nguvu hata ya kuomba na kuutafuta Uso wa Mungu wetu, Basi ni vema ukamshirikisha ndugu yako wa karibu sana kwa kadri Roho wa Mungu atakavyokuongoza ili akubebee mzigo wako katika maombi.
Bwana Yesu aliwaasa wanafunzi wake wakeshe wakiomba ili wasiingie majaribuni kwakuwa roho ila radhi ila mwili ni dhaifu. Maombi ndiyo silaha katika yote magumutunayokutana nayo siku zote za maisha yetu, na kwa Mungu hakuna gumu lolote asiloliweza.
Umuhimu wa kusamehe upo muda wote, ila si kusamehe tu bali kusamehe na kusahau maana Neno la Mungu linasema tazama ya kale yote wamepita na sasa yamekuwa mapya. Kwa hali ya kibinadamu ni ngumu sana hasa inapokuwa mtu anarudia kosa lile lile zaidi ya mara moja, na kwa jinsi hiyo tunakumbuka ni mara ngapi ambapo kosa hilo limekuwa likijirudia siku zote inatupa kuwa na wakati mgumu sana pia machungu moyoni, lakini Bwana Yesu amesema nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi hivyo tukimbilie kwake tupate pumziko.
Tatizo la kutosamehe toka moyoni ni la kila mtu katika ulimwengu wa sasa, lakini Neno la Mungu linatuasa kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote pamoja na huo utakatifu kwakuwa hakuna atakaye muona Mungu asipokuwa nao. Katika nyakati hizi, hatutakiwi kuweka hasira wala kinyongo kwakuwa hatujui lini Yesu atarudi kulinyakua kanisa au ni wakati gani kifo kitatukuta maana hakuna dhambi ndogo wala kubwa ila yoyote ile inatosha sana kukupeleka kwenye ziwa liwakalo moto milele na milele.
Kila tunapoomba Mungu anasikia, naye Baba yetu yuko tayari kutupa msaada muda na wakati wote kama tukikiri kutokuweza na kwenda mbele zake kwa toba ya kweli. Inatupasa kuwapenda adui zetu, kuwaheshimu na kujishusha kwako, yamkini tunatizama kibanzi ndani ya jicho la jirani badala ya kuitizama na kuitoa boriti kwenye jicho letu kwanza.
Mungu atusaidie siku zote tuishi maisha yanayompendeza yeye pamoja na wanadamu wote ili baraka zake zisitupungukie ila zitufikie hata zitupitilize, kwakuwa hatutachoka kutenda mema siku zote za maisha yetu.
Upendo na Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nasi siku zote za maisha yetu na Mungu atubariki sana.
Tujadiliane na kuelekezana njia sahihi ya kuurithi ufalme wa Mbinguni na uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.
Pages
Nataka Kuokoka Sasa Hivi!
Ndugu yangu, hakuna kilicho bora sana duniani na baada ya maisha haya zaidi ya roho yako? Je, unafahamu baada ya maisha ya hapa duniani kuna maisha mengine ambayo wewe una maamuzi ya asilimia mia kuchagua?
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.
Fahamu kuwa kuna Mbingu na Jehanamu. Mshahara wa dhambi daima ni mauti, na mshahara wa mema ni uzima wa milele. Chagua uzima ukaishi milele kwakuwa maisha ya hapa duniani ni ya kitambo kifupi sana nayo yamejaa masumbuko na taabu nyingi sana kila inapoitwa leo.
Yesu anakupenda sana, inawezekana kuna mtu anakupenda sana ila Yesu anakupenda zaidi ya wote duniani hivyo nakushauri ukate shauri umfuate yeye maana atakupa kustarehe milele na kuurithi ufalme wa mbinguni pamoja naye.
No comments:
Post a Comment