Mungu wetu ni Yule Yule jana, leo na hata milele. Habadiliki kwakuwa Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho.
Tunapokutana na shida, mtizamo wetu huwa ni namna gani kwa namna ya kibinadamu kwa nguvu, mali au maarifa yetu tunaweza kutatua tatizo, ambapo tunasahau kwamba hatuwezi neno lolote pasipo Mungu kuwa pamoja nasi. Maarifa ya binadamu kwa Mungu ni sawa na upumbavu!
Haijalishi katika nyakati hizi maarifa yamekua kiasi gani, ila ukweli ni kwamba bila pumzi ya Mungu sisi sio kitu chochote, pia maandiko yanasema mwanadamu ni udongo na kwenye udogo atarudi. Tukirejea pia Neno la Mungu linapotuambia nyakati hizi maarifa yanapoongezeka upendo wa wengi utapoa, na watu tutakuwa wenye kujipenda zaidi wenyewe, fedha, mali na anasa kuliko kumpenda Mungu.
Mungu ana namna nyingi sana za kutuongoza ikiwa pamoja na kuturudi kutokana na njia zetu mbaya ingawa katika uhalisia tunaona kwamba mengi tunayokutana nayo ni sehemu ya maisha ya kila siku ambayo yanampata yeyote yule ila wakati sasa umefika tumtizame Mungu katika uhalisia wake mkuu.
Mungu ni Yule Yule aliyemuongoza Yusufu katika magumu yote hadi kufikia ngazi ya juu ya utawala wa Misri, ndiye Yule Yule aliyembariki Jacob, akawavusha wana wa Israel kwenye bahari ya Sham, akawapa maji kwenye mwamba, akawashushia mana toka Mbinguni, aliyekuwa pamoja na Daudi mtumishi wake hata Daudi akamshida Goliati, ndiye aliyempatia Ibrahim mwana katika uzee wake.
Pia Mungu ndiye aliyeshusha gharika nyakati za Nuhu, pia akaiteketeza miji ya Sodoma na Gomora kutokana na kumuasi na kupitiliza kwenye dhambi kiasi cha kutisha.
Aliyetenda mema kipindi kile ndiye anayetenda pia anaweza kutenda leo hii, lakini tunapomuasi hawezi kuwa pamoja nasi hivyo mabaya yatatufika kwa urahisi sana. Mema yote hutoka kwa Mungu daima, kwakuwa yeye hutuwazia mema kila inapoitwa leo. Mabaya daima yanatoka kwa mwovu Shetani na malaika zake kwakuwa hiyo ndiyo asili yao.
Haijalishi ndugu yangu unasumbuka na kuteseka na mangapi; ila nakuambia leo kwamba usikate tamaa kumtumaini Mungu, maana pasipo imani haiwezi kumpendeza yeye hivyo ukiweka imani yako iwe thabiti mbele zake, daima utakwenda kuona uwepo wake kwako na Neno lake litakuongoza na baraka zikufike na kupitiliza kila uingiapo na utokapo.
Namna pekee ya kuongea na Mungu wetu ni kwa kupitia maombi, maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wakeshe wakiomba wasije kuingia majaribuni hivyo hatuna budi kuomba muda wote ili tufahamu Mungu ana mpango gani mbele yetu vinginevyo tutaenenda kama vipofu ambao wanajiongoza wenyewe na kuishia kwenye shimo.
Yamkini unathamini sana nyumba yako, gari, familia au kazi pengine elimu uliyonayo ila cha kusikitisha sana ni kwamba hakuna hata mmoja atakaye ondoka na kitu hata kimoja alichonacho hapa duniani wala kaviwezi kutusaidia kufika Mbinguni ila kwa kupitia Mwana pekee wa Mungu ambaye ni Yesu aliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Tuna mifano mingi ya watu matajiri na wenye elimu sana waliokufa, ila miili yao ilizikwa bila mali yoyote. Ni vema kujifunza sasa kwa mifano hai na tukumbushane daima. Solomon anasema mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu!
Kuna wakati utafika ambapo kile utakachokuwa nacho ni ile hazina tu uliyoiweka Mbinguni kwa Baba, sasa je, unatumia kiasi gani kwenye starehe na anasa za duniani ambazo zinapita tu? Kumbuka, pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu maana mkulima anapopanda mbegu anaamini kwamba udogo utaishikilia, mvua itanyesha na mazao yatashamiri walakini asingeamini hivyo asingepanda mbegu na kupoteza muda wake. Hebu kumbuka Ibrahim alimtoa mtoto pekee ambaye Mungu alimbariki naye katika uzee wake, lakini alijua kwamba Mungu alinipa hivyo hata nikimtolea atanipa tena.
Mimi na wewe si mali yetu wenyewe ila ni mali ya Mungu aliye hai, kwahiyo hatuna mamlaka wala ruhusa ya kufanya mambo yetu wenyewe ila kwa amri yake Yeye aliye Mkuu kuliko wote, maana kwa pumzi yake tunaishi, kwa neema na baraka zake tunafanikiwa daima. Usiogope wala kuwa na mashaka, ila amini kuwa Mungu habadiliki hivyo kama alitenda enzi zile, hata leo atatenda hivyo cha msingi ni kukaa katika Neno lake na kukua katika imani.
Baraka za Ibrahim, Isaka na Yakobo ziambatane nawe hata zikupitilize pamoja na vizazi vyako!