Maamuzi ni kitu cha msingi sana katika maisha ya mwanadamu hasa kama yanafanyika kwa Hekima, Busara pamoja na usahihi; kwanini? Kwasababu maamuzi unayoyafanya sasa itakubidi uishi matokeo yake baadaye. Ukiamua jambo Fulani, au usiamue vyovyote kwa namna hiyo bado unakuwa umefanya maamuzi hakika.
Waamuzi 16:17 – 21 Samsoni aliamua
kufanya maamuzi ya kuvunja unadhiri wake kwa Mungu kwasababu alimpenda sana
Delila, lakini hakika ilimgharimu Samsoni kusudi la Mungu ndani yake, macho
yake hata uhuru wake.Unaposhindwa kufanya maamuzi sahihi siku zote unakuwa
mtumwa.
Kati yetu kuna ambaye hajawahi kuwa
kwenye hali ambayo ni ngumu sana, kutokana na maamuzi yasiyofaa uliyoyafanya
hata akahisi kabisa kwamba ndani yako uwepo wa Mungu haupo kabisa kiasi kwamba hata
maombi yake ni kama yanamzunguka tu hayaendi popote?
Kuna dada zetu ambao wanadanganywa na
kina kaka ambao hata hawaeleweki kuwa na muelekeo mzuri wa maisha; ni pale
anapoambiwa tu “NAKUPENDA” anaona
vingine vyote havifai, kiasi cha kufikia hatua ya kuukimbia wokovu. Katika
maamuzi kama haya siku zote huwa hatuhesabu gharama kabla ya kuchukua hatua. Luka 14:28 – 30
Mwana Mpotevu aliamua kuchukua urithi
wake toka kwa baba yake, akaenda kuishi maisha ya anasa na kutumia mali zote
hata zikaisha; akaishia kwenye kazi ya kulisha nguruwe hata kutamani kushiriki
chakula na nguruwe. Luka 15:11 – 21
Ndio maana dhambi ni kitu kibaya sana,
kwani unakuja kujua na kujutia maamuzi uliyofanya baadaye, pia inatubidi
tufahamu kuwa si mara zote utajuta hapa duniani bali kuna wakati utajuta kwenye
moto wa milele.
Maamuzi ya Eva kula tunda la mti wa
ujuzi wa mema na mabaya pia akamshawishi mumewe Adam ambaye naye aliamua
kushiriki na mkewe viliwagharimu sana, ambapo kwa dhambi hiyo inatugharimu hata
sisi leo hii. Lakini, Bwana Yesu aliamua kuja duniani ateseke, afe na afufuke
ili sisi tupate msamaha wa dhambi kwa kupitia Yeye, hivyo badala ya sisi
kuhukumiwa tupate kuhesabiwa haki yote.Yohana
3:16 – 17
Isaya
46:10 Mungu pekee ndiye anayefahamu siri ya mambo yajayo, dakika chache
hata miaka kenda inayokuja mpaka milele yote. Siku zote tunapofanya maamuzi,
kama hatuongozwi na Roho wa Mungu hakika tuna nafasi kubwa sana ya kukosea na
kuishi katika majuto.
Kuna watu ambao wanafahamika kuwa na
busara pia Hekima sana za kibinadamu, ila hawa pia wamekosea na wataendelea
kukosema katika mambo tofauti tofauti kwani Mungu amewaficha wazee wenye Hekima
akawafunulia watoto wadogo. Mathayo
11:25
Ukiamka asubuhi anza na Yesu, ukitaka kufanya jambo mshirikishe Yeye wala usitizame urahisi wa jambo au mara ngapi umeshalifanya kwani sisi hukosea daima na haijalishi, ila Yesu ni yule yule jana leo na hata milele, na hajawahi wala haitatokea akakosea kamwe. Malachi 3:6